• HABARI MPYA

    Wednesday, November 02, 2016

    KICHUYA AWAPA RAHA SIMBA SC...STAND UNITED YAFA 1-0 KAMBARAGE

    Na Moses Isaac, SHINYANGA
    SIMBA SC wameendelea kulifukuzia kwa kasi taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya timu ngumu msimu huu, Stand United ya Shinyanga.
    Ushindi huo, unaifanya Simba SC ifikishe pointi 35 baada ya kucheza mechi 13, wakati Stand inabaki na pointi zake 22 za mechi 14. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa, Shomary Lawi wa Kigoma aliyesaidiwa na Mirambo Tshikungu na Robert Ruhemeja, Simba walipata bao lao mapema kipindi cha kwanza.
    Shizza Kichuya akipongezwa na wachezaji wenzake Mohamed Ibrahim kulia, Muzamil Yassin kushoto na Janvier Bokungu nyuma baada ya kufunga bao lake la 10 msimu huu katika Ligi Kuu

    Bao hilo lilifungwa na winga machachari wa Wekundu hao wa Msimbazi, Shizza Ramadhani Kichuya kwa penalti dakika ya 33 baada ya mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo kuangushwa na beki Adeyum Ahmed kwenye boksi.
    Baaada ya bao hilo, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini ni Simba SC waliokuwa waking’ara uwanjani.
    Mapema dakika ya nane, Kichuya aliunganishia nje kwa kichwa krosi ya beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kabla ya Nahodha wa Stand United, Jacob Massawe kupiga juu kufuatia krosi ya Frank Hamisi.
    Kipindi cha pili, mchezo uliendelea kuwa wa mashambulizi ya pande zote mbili, lakini Simba inayofundishwa na Mcameroon, Joseph Marius Omog ilifanikiwa kuulinda ushindi wake.
    Na Simba SC ilikaribia kupata bao la pili dakika ya 65 kama si kiungo Mohamed ‘Mo’ Ibrahim kupiga juu ya lango kufuatia pasi nzuri ya Kichuya.
    Kikosi cha Stand United kilikuwa; Frank Muwonge, Aaron Lulambo, Adeyum Ahmed, Erick Mlilo, Ibrahim Job, Pastory Athanas, Kelvin Kongwe, Jacob Massawe, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Frank Hamisi na Amri Kiemba.
    Simba SC; Vincent Angban, Janvier  Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Method Mwanjali, Juuko   Murshid, Jonas Mkude, Shizza Kichuya/Jamal Mnyate dk75, Muzamil Yassin, Laudit  Mavugo/Ibrahim Hajib dk87, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na Mwinyi Kazimoto/Mussa Ndusha dk79.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KICHUYA AWAPA RAHA SIMBA SC...STAND UNITED YAFA 1-0 KAMBARAGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top