• HABARI MPYA

    Sunday, November 13, 2016

    KAMA NI HUJUMA, SIMBA IMEHUJUMIWA NA VIONGOZI WAKE

    BAADA ya mwanzo mzuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikicheza mechi 13 bila ya kupoteza hata moja, upepo uligeuka ghafla na Simba SC ikaanza kuboronga.
    Ikitoka kukusanya pointi 35 katika mechi 13, kutokana na kushinda mara 11 na kutoa sare mbili, Simba SC ikajikuta ikipoteza mechi mbili za mwisho nyumbani na ugenini.
    Ilianza kufungwa 1-0 na African Lyon Novemba 6, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 2-1 na Prisons siku tatu baadaye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Kw matokeo hayo, gepu la pointi ilizokuwa inawazidi wapinzani, Yanga ambao pia ndio mabingwa watetezi likapungua kutoka nane hadi kubaki mbili ndani ya mechi mbili.
    Bahati nzuri Ligi Kuu ikawa imefikia tamati ya mzunguko wake wa kwanza na yanafuatia mapumziko marefu kidogo hadi katikati ya Desemba.
    Vinginevyo kama Ligi ingeendelea tutarajie mambo yangekuwa magumu zaidi kwa Simba SC.
    Na hii inataka kuwa desturi kwa takriban msimu wa nne sasa, Simba inakuwa na mwanzo mzuri katika Ligi Kuu, lakini baadaye upepo unageuka inapoteza mechi za kutosha kuwapisha Azam na Yanga mbele.
    Msimu uliopita ndiyo ilisikitisha zaidi, Ligi Kuu ikiwa inaelekea ukingoni Simba ilifikia wakati inaongoza Ligi kwa pointi 11 japokuwa wapinzani, Azam na Yanga walikuwa wana viporo viwili viwili.
    Mwishowe Simba ikamaliza nafasi ya tatu na kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) ikatolewa katika Robo Fainali na Coastal Union ya Tanga iliyoshuka Daraja. 
    Na kila baada ya matokeo mabaya ya kustaajabisha Simba SC hufuatia sababu za kwa nini yametokea hayo.
    Uongozi huibuka na sababu zile zile kila msimu kwamba kuna wachezaji wamehujumu timu kwa kutumiwa na wapinzani.
    Na wachezaji nao huibua sababu zile zile kwamba hawajalipwa stahiki zao, ikiwemo mishahara kwa muda mrefu.
    Kinachofuata nini? Simba inabomoa timu, wachezaji wazuri kama Hamisi Kiiza aliyekaribia kuwa mfungaji bora msimu uliopita wanaachwa na wanasajiliwa wengine wapya, nao wazuri tu kama Laudit Mavugo.
    Lakini tayari sasa wachezaji wapya hawafurahiani na uongozi wa Simba SC chini ya Rais wake, Evans Elieza Aveva – nini tutarajie? Kuachana tu hivi karibuni.
    Baada ya matokeo mabaya ya msimu huu, baadhi ya magazeti yakaripoti wachezaji wa Simba SC hawajalipwa mishahara miezi mitatu.
    Na kwa kuwa uongozi wa Simba haujajitokeza kukanusha habari hizo, ina maana tuamini kweli wachezaji wa timu hiyo hawajalipwa mishahara kwa miezi mitatu.
    Na miezi mitatu ni maana yake tangu Ligi inaanza Agosti wachezaji wa Simba SC hawajalipwa mishahara na hiyo inamaanisha, kwa wapya ambao ndio wengi tangu wameajiriwa wamekuwa wakiishi kwa fedha za usajili tu.
    Wachezaji wanapandishwa ndege kwa mechi za Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini, kumbe nyumbani familia zao zinalia njaa.
    Baadaye timu inakuja kufungwa mechi mbili mfululizo, hufikirii kwamba wale binadamu ujasiri wao wa kucheza mpira na matatizo umefikia kikomo, unawaza tu wamehujumu timu.
    Tuwe wawazi, hata hao viongozi wa Simba walikuwa waajiriwa na wengine ni waajiriwa hadi sasa – wanajua kwamba mtu ukicheleweshewa mshahara ufanisi unapungua kazini.
    Aveva alikuwa Meneja wa Embassy Hotel, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ hadi leo ni mtumishi wa Cargo Star – wote wanajua unapofanya bila kulipwa kwa wakati inaathiri utendaji wako.
    Moja ya sababu zilizochangia kushuka kwa elimu nchini ni Serikali kutozingatia suala la maslahi ya walimu – sasa tunatafuta mchawi wa nini kwa Simba SC kushuka ghafla wakati viongozi hawajali maslahi ya wachezaji?
    Hapa hakuna kisingizio ni uongozi umeshindwa majukumu yake – na wameona staili ya kuendesha timu ni kwa kuchangishana fedha kwenye magrupu ya watsap. Harusi watu wachange, misiba wachange na hata mpira pia timu ziendeshwe kwa michango na bado kuna watu wanajiita viongozi – wamekuwa viongozi wa vikoba au klabu za mpira?
    Wakati wa kuoneana haya umepitwa na wakati na sasa ni wakati wa kuambiana ukweli kwa manufaa klabu na michezo kwa ujumla.
    Haiwezekani wachezaji hawajalipwa mishahara miezi mitatu, timu haina mfadhili wala chanzo cha maana cha mapato – halafu viongozi wanasema timu imefungwa wachezaji wamehujumu.
    Kama ni hujuma, Simba imehujumiwa na viongozi wake ambao wameshindwa kuwalipa mishahara wachezaji hadi wakanyong’onyea na kufungwa mechi mbili mfululizo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMA NI HUJUMA, SIMBA IMEHUJUMIWA NA VIONGOZI WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top