• HABARI MPYA

    Sunday, November 06, 2016

    JUMA MAHADHI ASIPOSHITUKA MAPEMA YANGA SHAURI YAKE

    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katikati ya mwezi itasafiri hadi Zimbabwe kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa na wenyeji, The Warriors.
    Na kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ juzi ameita wachezaji saba kati ya 24 kutoka kikosi cha Simba SC, ambao ni beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, viungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Jonas Mkude, Muzamil Yassin, Shizza Kichuya, Jamal Mnyate na mshambuliaji ni Ibrahim Hajib.
    Simba SC ndiyo vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wakiwa wanaongoza kwa pointi zao 35 za mechi 13, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 27 za mechi 13 pia.
    Kutoka kikosi cha Yanga, Mkwasa amewachukua kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, mabeki Mwinyi Hajji, Vincent Andrew wa Yanga, Simon Msuva wa Yanga.
    Wachezaji wengine walioitwa Stars kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika Novemba 13 ni makipa; Said Kipao wa JKT Ruvu na Aishi Manula wa Azam FC.
    Mabeki; Erasto Nyoni, David Mwantika wa Azam FC, Michael Aidan wa JKT Ruvu na James Josephat wa Prisons.
    Viungo ni Himid Mao wa Azam FC na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting na washambuliaji John Bocco wa Azam FC, Elius Maguli wa Oman Club, Thomas Ulimwengu ambaye hajapata timu baada ya kumaliza mkataba wake TP Mazembe ya DRC na kundoka mwezi uliopita, Omar Mponda wa Ndanda FC na Nahodha Mbwana Samatta wa K.R.C Genk ya Ubelgiji.
    Wakati akitaja kikosi hicho, Mkwasa alisema kwa sababu mbalimbali hususani majeruhi, amewaacha wachezaji Shomary Kapombe wa Azam FC, Hassan Kabunda wa Mwadui FC, Juma Abdul na Juma Mahadhi wa Yanga.
    Inafahamika Kapombe wa Azam FC na Juma Abdul wa Yanga ni majeruhi, lakini Hassan Kabunda wa Mwadui FC na Juma Mahadhi wa Yanga wameachwa kwa sababu mbalimbali.
    Mkwasa ameziweka kwenye mabano sababu za kuwaacha wachezaji hao wawili chipukizi labda kwa kuwatunzia heshima.
    Lakini kwa sababu wamekuwa wakitumika katika klabu zao siku za karibuni ama kwa kutokea benchi au kuishia kukaa benchi, tukubaliane hawa si majeruhi bali wameachwa kwa sababu nyingine.
    Mahadhi na Kabunda wote wanatoka koo maarufu kisoka, Juma akifuata nyayo za wajomba zake Rashid, Habib, Waziri, Bakari na babu yake Omar Mahadhi ’Bin Jabir’ na Kabunda akifuata nyayo za baba yake, marehemu Salum Kabunda wote ni vijana wadogo.
    Na ni mwaka huu walianza kuitwa timu ya taifa pamoja na chipukizi wenzao akina Mo Ibrahim, Muzamil Yassin na Kichuya. Wakati huo, Kichuya, Ibrahim na Muzamil walikuwa wanatokea Mtibwa Sugar, Mahadhi alikuwa anatokea Coastal Union ya Tanga na Kabunda huko huko Mwadui.
    Lakini baada ya kuonekana kidogo Taifa Stars wakasajiliwa na timu za Dar es Salaam zenye maslahi mazuri, Simba na Yanga. Hata Kabunda alikaribia kusajiliwa Simba.
    Kichuya, Ibrahim na Muzamil wote kwa sasa ni wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Simba SC wakati Mahadhi si mchezaji wa kikosi cha kwanza na hana uhakika hata wa kuingia kutokea benchi.
    Na siku zijazo Mahadhi anaweza akajikuta hata benchi hakai tena na mwisho wa siku ataingia kwenye orodha ya wachezaji waliodumu kwa muda mfupi Yanga SC.
    Juma ni Mahadhi wa pili baada ya Waziri, kiungo pia aliyecheza Yanga akitokea Coastal Union pia. Lakini Mahadhi hakuwahi kuachwa Yanga, aliondoka mwenyewe kufuata maslahi mazuri zaidi Moro United.
    Mwenyewe Omar Mahadhi Jabir alikuwa kipa bora aliyedakia African Sports na Simba SC na mwaka 1973 akachaguliwa kombaini ya Afrika baada ya kufanya vizuri na timu ya taifa kwenye Michezo ya Afrika Lagos Nigeria.
    Waziri ni mtoto pekee wa Mahadhi angalau kacheza timu ya taifa ya wakubwa – Habib aliwahi kuitwa timu ya vijana wakati golikipa Rashid na kiungo Bakari wao usela uliwazidi na si ajabu hawakuwa na mafanikio.
    Kwa nini Waziri alifanikiwa zaidi ya ndugu zake? Kwa sababu alikuwa ana malengo ya kuwa mchezaji mkubwa, hivyo alijibidiisha na hakuwahi kulewa sifa.
    Sinza yote ambako wamekulia vijana hao, ukiwauliza watakuambia Rashid alikuwa kipa mzuri, hata Baker alikuwa fundi, lakini mwishowe watakuambia kwa nini walikwama.
    Habib amekulia Magomeni kwa sababu anazaliwa na mama tofauti na akina Rashid, Baker na Waziri kaka zao Tima, aliyekuwa mke wa beki zamani wa Simba, Omar Tamba.
    Na huyu Tima ndiye mama mzazi wa kiungo mpya wa Yanga, Juma Mahadhi.
    Waziri baada ya kusajiliwa tu Yanga, alikwenda moja kwa moja kucheza japokuwa aliwakuta viungo wazoefu kama akina Ally Mayay, Ally Yussuf ‘Tigana’, Mtwa Kihwelo na Sekilojo Chambua.
    Na hata Juma Mahadhi aliingia na nyota hiyo, kwani kocha Mholanzi Hans van der Pluijm alimkubali sana na akaanza kumpa nafasi mapema tu.
    Lakini baadaye akaanza kumuanzishia benchi na siku za karibuni amekuwa hamuinui kabisa kumuingiza uwanjani – tutarajie nini siku zijazo? Atakuwa wa jukwani.
    Vyema sasa Juma Mahadhi akajitazama na kujiuliza anakosea wapi. Na na vizuri akawatumia akina Kichuya kujiuliza wale wamewezaje na hata wanamuacha katika mbio za kuyakimbilia mafanikio zaidi kisoka.
    Vitu rahisi tu. Mfumo wa maisha yake ya sasa una majibu yote. Anafanyaje mazoezi, anapumzikaje, anafanya nini kujiongezea uelewa, au maarifa kisoka na je nafsi yake imetekwa na nini zaidi kwa sasa?
    Kwa wachezaji wa nchi za wenzetu hususan Magharibi mwa Afrika umri kama wa Juma chini ya miaka 20 ndiyo wa kucheza mpira na wengi tayari wanakuwa Ulaya katika umri huo.    
    Na wachezaji wetu sasa waache kasumba za kwamba Watanzania hawawezi kucheza Ulaya – kwa sababu Mwana Samatta anacheza Ligi Kuu ya Ubelgiji hivyo, wafikirie kufuata nyayo zao.
    Waziri alikuwa hapendi kukaa benchi. Siku moja alitolewa katika mechi anachechemea huku analia baada ya kuumia Taifa Stars ikicheza Mwanza. Baadaye nikakutana naye nikampa pole kwa maumivu yaliyomfanya alie, lakini akanijibu; “Sikuwa nalia kwa maumivu ya kuumia (kwa kuchezewa rafu uwanjani), nilikuwa ninalia kuondoka uwanjani mechi haijaisha, huwa inaniuma sana,”.
    Lakini Juma Mahadhi anaamkia benchi kila siku na yeye anaona sawa tu, huo ni mwanzo wa kufeli. Anapaswa kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza Yanga kama Kichuya alivyo tegemeo la Simba sasa, kwa sababu wote wana vipaji.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JUMA MAHADHI ASIPOSHITUKA MAPEMA YANGA SHAURI YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top