• HABARI MPYA

    Friday, November 11, 2016

    HANS POPPE: SIMBA INAFUNGIWA NJE YA UWANJA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imelalamika kwamba imefungwa mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kutokana na mbinu chafu zinazofanywa na wapinzani wao nje ya Uwanja.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema leo katika mazungumzo na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kwamba baada ya mwanzo mzuri katika Ligi Kuu, ikiwemo kuwazuia mabingwa watetezi, Yanga kwa sare ya 1-1 wapinzani wao wakaanza mchezo mchafu.
    “Hebu jiulizeni, Simba ni timu nzuri tangu mwanzo inacheza vizuri na kushinda, Tumecheza mechi na hao mabingwa, tukiwa pungufu baada ya Mkude (Jonas) kutolewa kwa kadi nyekundu, lakini tukasawazisha bao na refa akakataa bao letu lingine. Iweje ghafla tufungwe mechi mbili mfululizo?”alihoji Hans Poppe.
    Zacharia Hans Poppe amesema Simba inafungiwa nje ya Uwanja  

    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) alisema kuna mbinu chafu zinazofanywa na wapinzani wao na hayo yamekuwa yakijirudia kwa miaka mitano sasa, jambo ambalo ni hatari kwa soka ya Tanzania.
    “Tena huwa wanatuambia kabisa, mnapigwa. Na kweli tunapigwa. Kwa sababu wanakuwa wanajua wamekwishakamilisha mbinu zao chafu. Huu si mpira na hatuwezi kufika popote,”alilalamika Poppe.
    Simba SC ilianza vyema Ligi Kuu na kuongoza kwa muda mrefu ikicheza mechi 13 bila kupoteza, ikishinda 11 na sare mbili.
    Lakini ghafla kibao kikageuka kwenye raundi mbili za mwisho na timu hiyo ikapoteza mechi mbili mfululizo, ikifungwa 1-0 African Lyon Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na 2-1 na Prisons Uwanja wa Sokoine Mbeya.
    Kwa sababu hiyo, Simba SC ikamaliza mzunguko wa kwanza inaongoza kwa pointi mbili tu zaidi dhidi ya mabingwa watetezu, Yanga (35-33) kutoka tofauti ya pointi nane.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE: SIMBA INAFUNGIWA NJE YA UWANJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top