• HABARI MPYA

    Wednesday, November 09, 2016

    AZAM FC YAMUENZI MZEE SAID KWA KUIPA 4-1 MWADUI FC

    Na Mwandishi Wetu, MWADUI
    TIMU ya Azam FC jioni ya leo imemuenzi vema aliyekuwa Mwenyekiti wake, Mzee Said Mohamed Abeid, aliyefariki dunia juzi jioni, kwa kuipa dozi kali ya mabao 4-1 Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Mwadui, Shinyanga.
    Azam FC hivi sasa ipo kwenye majonzi baada ya kuondokewa na kiongozi muhimu ndani ya timu hiyo, ambaye tayari maziko yake yamefanyika jana jioni kwenye makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.
    Katika kutoa ishara za maombolezo, wachezaji wa timu zote mbili pamoja na watu waliohudhuria mchezo huo walisimama kwa dakika moja, tukio lililofanyika kwenye mechi zote za ligi zilizofanyika leo lililoambatana na wachezaji kuvaa vitambaa vyeusi kwenye mkono mmoja.
    Iliwachukua Azam FC hadi kipindi cha pili kuweza kuandikisha ushindi huo mnono baada ya wenyeji Mwadui kutangulia kupachika bao la uongozi dakika ya 30 lililofungwa na Hassan Kabunda.
    Kabla ya kuingia bao hilo, mshambuliaji wa Mwadui Jerry Tegete dakika ya 19 alizua kizaazaa baada ya kufunga bao kwa mkono, ambalo lilikubaliwa na mwamuzi Enock Onoka, lakini baadaye alilikataa baada ya kushauriana na wasaidizi wake kufuatia wachezaji wa mabingwa hao kulilalamikia, jambo ambalo lilimfanya kuwalima kadi za njano Tegete na Abdallah Mfuko na kuamuru faulo ipigwe kuelekea lango la Mwadui.
    Azam FC ililazimika kufanya mabadiliko ya kwanza mchezoni dakika ya 36 baada ya kiungo Mudathir Yahya kuumia na nafasi yake ilichukuliwa na winga machachari Ramadhan Singano ‘Messi’ na hadi mpira huo unaenda mapumziko Mwadui ilitoka kifua mbele kwa bao hilo.
    Kipindi cha pili Azam FC ilirejea mchezoni na kuanza kuonyesha kandanda safi baada ya mabadiliko ya kuingia washambuliaji wawili Francisco Zekumbawira na Shaaban Idd, ambao waliongeza kasi kwenye eneo la ushambuliani la mabingwa hao.
    Shambulizi kali ililofanya Azam FC dakika ya 54 lilizaa bao la kusawazisha kwa timu hiyo, lililofungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, aliyepiga shuti kali lililomshinda kipa wa Mwadui. Bao hilo linamfanya Bocco kutimiza mabao sita msimu huu.
    Mwadui iliyoshindwa kabisa kuwadhibiti washambuliaji wa Azam FC hasa Shaaban na Zekumbawira, ilijikuta ikipigwa bao la pili na Shaaban dakika ya 71 kabla ya Zekumbawira kupigilia msumari wa tatu dakika ya 74 akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na kinda huyo.
    Shaaban aliendeleza moto wake kwa kuipatia bao la nne Azam FC dakika ya 77 baada ya kuwatoka walinzi kadhaa wa Mwadui na kupiga shuti lililomshinda kipa na hivyo kuhitimisha ushindi huo mnono kabisa kwa timu hiyo msimu huu.
    Katika mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, alianza kutumikia adhabu yake ya kutokaa benchi baada ya kutolewa nje na mwamuzi katika mechi iliyopita dhidi ya Mbao, hivyo benchi la mabingwa hao leo lilitawaliwa na Kocha Msaidizi, Yeray Romero.
    Ushindi huo unaifanya Azam FC kumaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa wenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ikijikusanyia pointi 25 ikizidiwa 10 tu na vinara Simba waliojikusanyia 35, ambao jioni ya leo wamepoteza mchezo kwa kufungwa na Tanzania Prisons mabao 2-1.
    Kikosi cha Azam FC leo kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael/Shaaban dk 46, Daniel Amoah, Aggrey Morris, Himid Mao, Mudathir Yahya/Singano dk 36, Salum Abubakar, Frank Domayo/Zekumbawira dk 54, John Bocco (C), Bruce Kangwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAMUENZI MZEE SAID KWA KUIPA 4-1 MWADUI FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top