• HABARI MPYA

    Tuesday, November 15, 2016

    AZAM FC WAIFUMUA RUVU SHOOTING 3-1 MECHI YA KUJARIBU WACHEZAJI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imemaliza programu ya kukifanyia tathimini kikosi chake kwa kuichapa Ruvu Shooting mabao 3-1, katika mchezo wa kirafiki uliomalizika usiku wa jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Mchezo huo ni wa pili mfululizo baada ya Jumamosi iliyopita kukipiga na JKT Ruvu, mechi zote hizo zikitumika kukiangalia kikosi hicho wakiwemo wachezaji tisa wanaofanya majaribio ndani ya kikosi hicho kwa ajili ya kupigania nafasi za kusajiliwa kwenye usajili wa dirisha dogo.
    Wachezaji wanaojaribiwa ni mabeki wa kati Nkot Mandeng Eric (Coton Sport De Garoua, Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Asec Mimosa, Ivory Coast), kiungo mkabaji Kingue Mpondo Stephane (Coton Sport Garoua, Cameroon) na Abdallah Khamis.
    Wachezaji waliopo majaribio Azam FC wakipongezana kwa ushindi wa jana
    Enock Atta Agyei (kulia) akimtoka beki wa Ruvu Shooting

    Washambuliaji ni Yaya Anaba Joel (Coton Sport Garoua, Cameroon), Samuel Afful (Sekondi Hasaacas, Ghana), Bernard Ofori (Medeama, Ghana), Konan Oussou (Tala’ea El-Gaish SC, Misri) na Jean Karekezi.
    Mabao ya Azam FC yamefungwa kiufundi na Bernard Ofori dakika ya nne akimalizi kwa kichwa krosi safi iliyochongwa na Gadiel Michael kabla ya Khamis Mcha kupiga la pili dakika ya 20 kwa njia ya penalti kufuatia Enock Atta Aggyei kuangushwa ndani ya eneo la hatari na kipa wa Ruvu Shooting, Bidii Hussein.
    Straika Afful aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ramadhan Singano ‘Messi’ alipigilia msumari wa mwisho kwenye lango la Ruvu Shooting kwa kufunga bao la zuri dakika 76, akipiga shuti kali pembeni ya uwanja lililomshinda kipa na kujaa wavuni.
    Mashabiki waliohudhuria mchezo wa leo kwa kiasi kikubwa wameridhishwa na uwezo alioonyesha Afful pamoja na winga Enock Atta Agyei, ambaye aliiweka katika wakati mgumu safu ya ulinzi ya Ruvu Shooting kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha, ambapo hata alipotolewa nje dakika ya 82, mashabiki walimpigia makofi kuashiria wamemkubali.
    Beki wa kulia wa Azam FC, Shomari Kapombe, naye alirejea dimbani baada ya kupona majeraha yake ya nyama za paja yaliyokuwa yakimsumbua, ambayo yamemfanya akae nje ya dimba kwa taktribani miezi miwili, ambapo aliingia uwanjani dakika ya 78 kuchukua nafasi ya Khamis Mcha.
    Mara baada ya mchezo huo, muda wowote kuanzia sasa benchi la ufundi la Azam FC linatarajia kutoa tathimini ya kikosi hicho pamoja na wachezaji waliokuwa kwenye majaribio ya nani asajiliwe na nani atemwe katika usajili huu wa dirisha dogo.
    Kikosi cha Azam FC tayari kimeshapewa likizo ya wiki mbili kuanzia leo mara baada ya mechi, ambapo kwa mujibu wa programu ya benchi la ufundi kikosi hicho kitaanza tena mazoezi ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi na michuano mingine Desemba 3  mwaka huu.
    Kikosi cha Azam FC hivi: Mwadini Ally, Gadiel Michael/Aggrey Morris dk 78, Kone Nabil Ibrahim, 46 Nkot Mandeng Eric, 17 Kingue Mpondo Stephane/Yaya Joel dk 62, Abdallah Khamis/Jean Mugiraneza dk 60, Ramadhan Singano/Samuel Afful dk 46, Khamis Mcha/Salum Abubakar dk 78, Enock Atta Agyei/Jean Karekezi dk 82, Konan Oussou/Mudathir Yahya dk 60, 27 Bernard Ofori/Shomari Kapombe dk 78.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC WAIFUMUA RUVU SHOOTING 3-1 MECHI YA KUJARIBU WACHEZAJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top