• HABARI MPYA

  Tuesday, October 18, 2016

  YANGA YATUA MWANZA BILA WATATU KUIVAA TOTO AFRICANS KESHO KIRUMBA

  Na Princess Asia, MWANZA
  MABINGWA watetezi, Yanga SC wamewasili mjini Mwanza asubuhi ya leo kwa ndege bila ya wachezaji wake watatu, kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, beki Juma Abdul na mshambuliaji Malimi Busungu.
  Yanga imetua Mwanza kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho dhidi ya wenyeji, Toto Africans mjini Mwanza na watatu hao wamebaki Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali.
  Barthez aliumia Oktoba 1 kwenye mechi na Simba, Juma Abdul aliumia kwenye mechi na Azam FC Jumapili wakati Malimi Busungu anadai ana matatizo ya kifamilia ingawa inasemekana anashinikiza kuruhusiwa kuondoka baada ya kuona hapati nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza. 
  Wachezaji waliowasili na timu mjini Mwanza ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Beno Kakolanya, mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Hajji, Pato Ngonyani, Oscar Joshua, Andrew Vincent, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan. 
  Viungo ni Saidi Juma ‘Makapu’, Juma Mahadhi, Simoni Msuva, Yussuf Mhilu, Mbuyu Twite, Thabani Kamusoko, Deus Kaseke na Haruna Niyonzima wakati washambuliaji ni Obrey Chirwa, Matheo Anthony, Amisi Tambwe na Donald Ngoma. 
  Yanga itakuwa na mechi mbili mfululizo Kanda ya Ziwa, kwani baada ya kumalizana na Toto kesho, Jumamosi itakuwa Uwanja wa Kaitaba kumenyana na wenyeji Kagera Sugar.
  Kwa ujumla Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho Azam FC wakiikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex, Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Ndanda FC wataikaribisha Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Prisons watakuwa wenyeji wa Stand United Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
  Mechi nyingine za Jumatano, African Lyon wataikaribisha Maji Maji Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Alhamisi Simba SC watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Uhuru na JKT Ruvu wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mabatini.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YATUA MWANZA BILA WATATU KUIVAA TOTO AFRICANS KESHO KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top