• HABARI MPYA

    Wednesday, October 12, 2016

    YANGA YAAMSHA HASIRA, YAITANDIKA 3-1 MTIBWA..CHIRWA AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO JANGWANI

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imezinduka baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo wa kwanza ndani ya mechi tatu ikitoka kufungwa 1-0 na Stand United na kulazimishwa sare ya 1-1 na mahasimu SImba SC umerejesha matumaini kwa mabingwa hao watetezi. 
    Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na winga Mzambia, Obrey Chirwa ambaye leo alichezeshwa kama mshambuliaji pacha wa Amissi Tambwe.
    Wachezaji wa Yanga wakimpongeza Ngoma baada ya kufunga bao la tatu leo
    Obrey Chirwa kulia akiwania mpira dhidi ya Cassian Ponera wa Mtibwa


    Amissi Tambwe akimruka beki wa Mtibwa, Issa Rashid 'Baba Ubaya'

    Chirwa aliyesajiliwa msimu huu kutoka FC Platinums ya Zimbabwe, alifunga bao hilo kwa shuti akiwa ndani ya boksi akimalizia mpira ulioparazwa kwa kichwa na beki Andrew Vincent ‘Dante’ baada ya krosi ya winga Simon Msuva.
    Yanga ingeweza kumaliza kipindi cha kwanza inaongoza kwa mabao zaidi, iwapo ingetumia vyema nafasi zaidi ya tatu nzuri ilizotengeneza za kufunga.
    Kipindi cha pili, kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm alianza na mabadiliko akimpumzisha Deus Kaseke na kumuingiza Geoffrey Mwashiuya.
    Pamoja na mabadiliko hayo, Yanga walijikuta wakiwaruhusu Mtibwa Sugar kusawazisha bao kupitia kwa winga wa zamani wa Simba SC, Haroun Chanongo dakika ya 63 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Tinocco.
    Yanga wakatulia na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 68 kupitia kwa Msuva kabla ya mshambuliaji aliyetokea benchi Donald Ngoma kufunga la tatu dakika ya 80 akimalizia kazi nzuri ya Mwashiuya. 
    Yanga ikalazimika kumalizia pungufu mchezo huo baada ya mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe kugongana na Shaaban Nditi na kupasuka kwenye dakika ya 87.
    Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi saba, inazidiwa pointi sita na mahasimu wao wa jadi, Simba SC walio kileleni ingawa wamecheza mechi moja zaidi. 
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Vincent Andrew, Kevin Yondan, Said Juma ‘Makapu’/Mbuyu Twite dk74, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amisi Tambwe, Obrey Chirwa/Donald ngoma dk73 na Deus Kaseke/Geoffrey Mwashiuya dk46.
    Mtibwa Sugar; Benedicto Tinocco, Rogers Gabriel, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Cassian Ponera, Dickson Daudi, Shaaban Nditi, Ally Makalani, Mohammed Issa, Rashid Mandawa, Ibrahim Rajab ‘Jeba’/Hussein Javu dk66 na Haruna Chanongo/Kelvin Friday dk75.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAAMSHA HASIRA, YAITANDIKA 3-1 MTIBWA..CHIRWA AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top