• HABARI MPYA

    Sunday, October 16, 2016

    YANGA NA AZAM ZAZIDI KUJICHUJA MBIO ZA UBINGWA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    YANGA na Azam FC zimezidi kujitoa katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kutoa sare ya 0-0 katika mchezo baina yao jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Matokeo hayo yaliyopokewa kwa furaha na wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Simba SC yanazifanya timu hizo zilizokuwa zikitawala soka ya Tanzania kwa miaka minne iliyopita ziendelee kusuasua katika Ligi Kuu.
    Yanga inafikisha pointi 15 baada ya mechi nane, ikitoa sare ya tatu, baada ya kufungwa mechi moja na kushinda nne, wakati Azam FC inafikisha pointi 12 baada ya kucheza mechi tisa, ikitoa sare ya tatu baada ya kufungwa mechi tatu na kushinda tatu – wakati Simba SC yenye pointi 23 za mechi tisa kutokana na kushinda mara saba na sare mbili, inagonoza Ligi Kuu.
    Wachezaji wa Yanga na Azam wakiwani mpira wa juu leo

    Katika mchezo huo, timu zote zilishambuliana kwa zamu na Yanga ndiyo waliokuwa wa kwanza kulitia majaribu lango la Azam FC dakika ya kwanza tu kufutia kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko kupiga shuti kali liliookolewa na kipa Aishi Manula na kuwa kona ambayo iliokolewa pia.
    Winga Muivory Coast wa Azam, Ya Thomas Gonza aliunganishia nje krosi ya Erasto Nyoni dakika ya 13 na dakika ya 16 Mzambia Obrey Chirwa alimdakisha mpira wa kichwa Manula kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Juma Abdul.
    Kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’ aliokoa shuti la kiugo wa Azam, Mudathir Yahya dakika ya 23 na kuna ambayo haikuwa na madhara.
    Yanga ilipata pigo dakika ya 31 baada ya beki wake tegemeo wa kulia, Juma Abdul kuumia kufuatia kugongana na Kangwa dakika ya 27 na kushindwa kuendelea na mchezo baada ya matibabu ya takriban dakika tatu, nafasi yake ikichukuliwa na Mbuyu twite.
    Kiungo wa Azam, Mudathir Yahya akimiliki mpira mbele ya kiungon wa Yanga, Thabani Kamusoko 
    Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma akienda juu kupiga mpira kichwa 
    Mashabiki wa Yanga wakiwa hawaamini macho ya leo Uwanja wa Uhuru

    Nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’ alifumua shuti kali dakika ya 41 ambalo hata hivyo liliokolewa na Dida. Yanga wakajibu dakika ya 44 kwa Chirwa kuunganisha krosi ya winga Simon Msuva, lakini Manula akaokoa.
    Dida akaokoa shuti la Kangwa dakika ya 55 baada ya Azam kupandisha shambulizi zuri la haraka.
    Azam ilipata pigo nayo dakika ya 78 baada ya Bocco kushindwa kuendelea na mchezo kufuatia kugongana na beki wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ na nafasi yake ikachukuliwa na Mzimbabwe Francesco Zekumbawira.  
    Dakika mbili baadaye Dante naye akashindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia kufuatia kugongana na kiungo wa Azam, Himid Mao ‘Ninja’ na nafasi yake kuchukuliwa na Nahodha, Nadir Haroub 'Cannavaro'. 
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Bruce Kangwa/Khamis Mcha ‘Vialli’ dk87, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Daniel Amoah, Jean Baptiste Mugiraneza, Himid Mao, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco/Francesco Zekumbawira dk78 na Ya Thomas Gonazo.
    Yanga SC; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul/Mbuyu Twite dk31, Mwinyi Hajji, Andrew Vincent/Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dk80, Kevin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Deus Kaseke/Geoffrey Mwashiuya dk57. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA NA AZAM ZAZIDI KUJICHUJA MBIO ZA UBINGWA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top