• HABARI MPYA

  Monday, October 10, 2016

  TASWA WAANDAA KONGAMANO LA MABADILIIO YA MIFUMO SIMBA NA YANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeandaa kongamano maalum Oktoba 20 mwaka huu kuzungumzia kuhusiana na mifumo ya kiuendeshaji ambayo klabu kongwe nchini za Simba na Yanga zipo mbioni kuingia.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, 
  Katibu Mkuu TASWA, Amir Mhando amesema kwamba kongamano hilo linatokana na klabu za Simba na Yanga, hivi sasa katika mchakato wa kubadilisha mfumo wao wa kiundeshaji.
  Amesema Simba inataka kuingia utaratibu wa hisa, wakati Yanga inataka kukodishwa na TASWA inaamini yapo mambo ambayo pengine wanachama, mashabiki na hata wadau wa mpira wa miguu na wanamichezo kwa ujumla wanapaswa kufahamu kwa undani zaidi kuhusiana na mifumo hiyo miwili ili kuwe na uelewa mpana zaidi.
  Ili kufanikisha mdahalo huo ambao ukumbi utakaofanyika utatangazwa hivi karibuni, TASWA imeunda Kamati ya watu sita kusimamia ambao ni Frank Sanga ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Juma Pinto (Mwenyekiti TASWA) na Asha Muhaji (Mhariri wa michezo gazeti la Rai).
  Wengine ni Florian Kaijage (Mhariri Mipango Azam TV), Amir Mhando (Mhariri gazeti la Spoti Leo na Katibu Mkuu TASWA na Shija Richard Mhazini Mkuu TASWA.
  Mapendekezo ya awali kuhusu washiriki wa kongamano hilo inatarajiwa lihusishe wataalamu kwenye sekta ya michezo, wahariri wa habari za michezo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ofisi ya Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
  Wengine ni wanasheria, wataalamu wa masuala ya hisa, viongozi wa klabu hizo na baadhi ya wadau muhimu wa soka nchini, wakiwemo viongozi wa soka wa zamani katika ngazi mbalimbali.
  Hata hivyo, Amir amesema kikao cha kamati hiyo kitakachofanyika kesho Jumanne kitaandaa utaratibu mzima wa kongamano hilo, ikiwemo kupanga waalikwa na namna ya uendeshaji utakavyokuwa na lengo pia liwe live (mubashara) katika televisheni ili wadau wengi zaidi wafuatilie.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TASWA WAANDAA KONGAMANO LA MABADILIIO YA MIFUMO SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top