• HABARI MPYA

  Sunday, October 09, 2016

  SIMBA SC WACHOSHWA NA DANADANA ZA SUALA LA KESSY

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
  KLABU ya Simba SC imesema kwamba imechoshwa na danadana za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu mustakabali wa suala la beki wao, Hassan Ramadhani Kessy, ambaye amesajiliwa na mahasimu wao, Yanga kinyume cha sheria.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe aliiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana kwamba mara ya mwisho TFF iliwaambia suala hilo lingemalizwa ndani ya Septemba, lakini sasa Oktoba inayoyoma na hakuna hatua iliyochukuliwa. 
  Alisema kwamba katika kikao cha mwisho walikubaliana na Yanga SC kuwaomba Mawakili Said El Maamry na Profesa Mgongo Fimbo kuwasimamia katika cha kutafuta suluhisho la suala hilo.
  Hans Poppe amesema kwamba wamechoshwa na danadana za suala Kessy

  Poppe alisema kikao hicho kilifuatia agizo la Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwapa siku tatu kuanzia Septemba 24, 2016 kumaliza wenyewe suala hilo, hatua ambayo ilifikiwa baada ya mjadala wa muda mrefu kuhusu kesi mbili zilizofunguliwa na Simba mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Richard Sinamtwa. 
  Kesi hizo ni Yanga kudaiwa kuingia mkataba na Kessy wakati bado ana mkataba na Simba SC nay a pili ni mchezaji huyo kudaiwa kuanza kufanya mazoezi pia kusajili Yanga na kwenda nje ya nchi wakati akiwa ndani ya klabu yake hiyo ya zamani. 
  Poppe alisema kwamba kwa sababu tangu wiki iliyopita wamekuwa wakipigwa danadana na TFF na Yanga juu ya suala hilo, wanaona bora lirudishwe kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji limalizwe huko.
  “Kama Yanga wangekuwa wanataka suala hili liishe mapema wagetumia kipindi hiki kukutana nasi mbele ya hap wakubwa (El Maamry na Mgongo Fimbo) ili tulimalize, lakini wamekuwa kimya muda wote huu, maana yake hawako tayari, hivyo hili suala ni bora lirudie Kamati ya Sheria,”alisema. 
  Wakati inatoa agizo la kuzitaka klabu hizo zimalizane zenyewe, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ilisema kwamba kama hawatafikia mwafaka katika siku tatu walizopewa, mashauri hayo yatarudi mbele ya kamati na kufanya uamuzi kwa mujibu wataratibu, kanuni na sheria zinazoongoza mpira wa miguu Tanzania. 
  Ikumbukwe katika madai yake, Simba inataka ilipwe dola za Kimarekani 600,000, zaidi ya Sh. Bilioni 1.2 za Tanzania.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC WACHOSHWA NA DANADANA ZA SUALA LA KESSY Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top