• HABARI MPYA

  Saturday, October 15, 2016

  SIMBA SC HAWAKAMATIKI, HUYO KICHUYA ACHANA NAYE KABISA!

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jioni ya leo.
  Shizza Ramadhani Kichuya amekuwa nyota wa mchezo kwa mara nyingine, akiseti bao la kwanza kabla ya kufunga mwenyewe la pili katika ushindi huo.
  Ni ushindi ambao unawafanya vijana wa Joseph Marius Omog, kocha Mcameroon wafikishe pointi 23 baada ya kucheza mechi tisa za Ligi Kuu, wakiendelea kuongoza kwenye msimamo.

  Wachezaji wa Simba SC wakifurahia ushindi wao wa leo dhidi ya Kagera Sugar

  Nyota wa Simba, Shizza Kichuya akipiga shuti pembeni ya beki wa Kagera Sugar
  Beki wa Simba SC, Mohammed Hussein 'Tshabalala' akimtoka mchezaji wa Kagera Sugar

  Simba SC ilipata bao lake la kwanza dakika mbili kabla ya mapumziko, mfungaji kiungo Muzamil Yassin aliyemalizia kwa kichwa kona ya winga Shizza Ramadhani Kichuya.
  Mshambuliaji mpya kutoka Ivory Coast, Frederick Blagnon ameendelea kucheza nyuma ya bahati yake baada ya leo pia kukosa mabao ya wazi kabla ya kutolewa anachechemea kumpisha Mrundi, Laudit Mavugo kipindi cha pili.
  Blagnon aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC, alikosa bao la wazi dakika ya 10 baada ya kupiga shuti lililokwenda nje akiwa amebaki na kipa Hussein Sharrif ‘Cassillas’.
  Mkongwe Danny Davis Mrwanda aliikosesha bao Kagera Sugar dakika ya 22 baada ya kutuliza mpira vizuri kifuani ndani ya boksi, lakini ukaokolewa na Juuko Murshid wakati anajiandaa kupiga. 
  Kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto naye akapoteza nafasi ya kufunga dakika ya 37 baada ya kuunganishia nje ya lango la Kagera krosi ya Kichuya kutoka upande wa kulia.
  Nyota wa Simba SC, Ibrahim Hajib Migomba hakuwa katika kiwango chake na leo na dakika ya 53 alipiga juu ya lango kabla ya kutolewa kumpisha Mohamed Ibrahim.
  Mavugo naye akapoteza nafasi mbili za kufunga kipindi cha pili, kwanza alipiga nje pembeni dakika ya 65 na dakika ya 69 akapiga juu akiwa ambeaki na kipa.
  Kichuya akafunga mwenyewe kwa penalti dakika ya 75 kuipatia Simba bao la pili baada ya beki Juma Ramadhani kumuangusha kwenye boksi Mohammed ‘Mo’ Ibrahim.
  Hilo linakuwa bao lake la nane Kichuya katika mechi 15 za mashindano yote tangu amejiunga na Simba msimu huu kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.
  Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Vincent Angban, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shizza Kichuya, Muzamil Yassin, Frederick Blagnon/Laudit Mavugo dk56, Ibrahim Hajib/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk60 na Mwinyi Kazimoto/Said Ndemla dk84.
  Kagera Sugar; Hussein Sharrif ‘Cassilas’, Mwahita Gereza, Godfrey Taita, Juma Ramadhan, George Kavilla, Suleiman Mangoma, Ally Nassoro, Shaaban Sunza, Danny Mrwanda/Themi Felix dk62, Edward Christopher/Paul Ngway dk62 na Mbaraka Abeid/Ally Ramadhani dk38.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC HAWAKAMATIKI, HUYO KICHUYA ACHANA NAYE KABISA! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top