• HABARI MPYA

    Monday, October 10, 2016

    PLUIJM: KOCHA WA YANGA MIMI, HUYO MWINGINE WA MAGAZETI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amesema kwamba hahofii chochote kuhusu mabadiliko ya benchi la Ufundi yanayozungumzwa na anaelekeza nguvu zake kwenye kuiandaa timu hiyo kwa ajili ya mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar keshokutwa. 
    Yanga watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar keshokutwa katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Pluijm amesema anafahamu umuhimu wa kushinda mchezo huo.
    Pluijm amesema anaelekeza nguvu zake kwenye maandaalizi ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar keshokutwa 

    “Nimesoma kwenye magazeti jana na leo, lakini sijali hizo taarifa. Mwajiri wangu hajaniambia chochote kuhusu hizo taarifa, mimi ninaendelea na kazi zangu kuiandaa timu kwa ajili ya mechi,”amesema Pluijm leo akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE.
    Na kuhusu mchezo wa keshokutwa, Pluijm alisema awali alikuwa anajua ni Alhamisi, lakini leo ndiyo kaambiwa kwamba mechi Jumatano.
    Hata hivyo, Mholanzi huyo amesema hana namna nyingine zaidi ya kujiandaa kwa mchezo huo ambao ni muhimu kushinda ili kurejesha imani ya mashabiki katika mbio za kutetea ubingwa.
    Habari za ndani kutoka Yanga, zinasema kwamba benchi lote la Ufundi la litaondolewa na watakuja watu kabisa baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
    Kocha Mkuu, Pluijm na wasaidizi wake, Juma Mwambusi, kocha wa makipa Juma Pondamali na Meneja Hafidh Saleh wote wazalendo wataondoka na Mzambia, George Lwandamina atakuwa Kocha Mkuu, akisaidiwa na wazalendo Charles Boniface Mkwasa, Manyika Peter kocha wa makipa na Meneja, Sekilojo Chambua.  
    Pluijm amejikuta katika wakati mgumu baada ya Yanga kuambulia pointi 11 kati ya 18 za mechi sita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Yanga SC imetoa sare mbili, imefungwa mechi moja na kushinda tatu tangu kuanza kwa Ligi Kuu – hiyo ikiwa ni mbali na kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii mbele ya Azam kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2.
    Na baada ya mchezo wa Oktoba 1, wakilazimishwa sare ya 1-1 na mahasimu, Simba SC waliokuwa pungufu kwa sehemu kubwa kufuatia Nahodha wao, Jonas Mkude kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 29, baadhi ya viongozi wa Yanga wamependekeza mwalimu huyo aondolewe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM: KOCHA WA YANGA MIMI, HUYO MWINGINE WA MAGAZETI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top