• HABARI MPYA

    Friday, October 07, 2016

    MKWASA: KURUDI YANGA POA TU, WAMALIZANE NA TFF

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba hana shida kurejea Yanga, iwapo klabu hiyo itafuata taratibu za kumuomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana, Mkwasa alisema kwamba amesikia taarifa za kutakiwa kurejea Yanga, lakini hajazipokea rasmi kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo.
    Na hata hivyo, Mkwasa alisema kwa kuwa yeye ana Mkataba na TFF wa kufundisha timu ya taifa – basi uongozi wa Yanga utalazimika kufuata taratibu ili kumpata.
    “Mimi sina tatizo na Yanga. Ndiyo imenifikisha hapa, nikianza kuitumikia kama mchezaji na baadaye kocha. Na nilikuja Taifa Stars nikitoka Yanga. Hivyo sina shida kabisa kurudi kule, ia wafuate tu taratibu kama kweli wananitaka. Waongee tu na TFF,”alisema. 
    Kocha Mkuu wa sasa wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm yupo katika wakati mgumu kufuatia timu kuambulia pointi 11 kati ya 18 za mechi sita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Charles Boniface Mkwasa amesema kwamba hana shida kurejea Yanga, iwapo klabu hiyo itafuata taratibu

    Yanga SC imetoa sare mbili, imefungwa mechi moja na kushinda tatu tangu kuanza kwa Ligi Kuu – hiyo ikiwa ni mbali na kupoteza mchezo wa Ngao ya Jamii mbele ya Azam kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2.
    Na baada ya mchezo wa Jumamosi wakilazimishwa sare ya 1-1 na mahasimu, Simba SC waliokuwa pungufu kwa sehemu kubwa kufuatia Nahodha wao, Jonas Mkude kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 29, baadhi ya viongozi wa Yanga wamependekeza mwalimu huyo aondolewe.
    Kamati ya Utendaji ya Yanga inaweza kukutana wiki hii kujadili benchi la Ufundi la timu kwa ujumla, baada ya malalamiko mengi kuhusu kuporomoka kwa kiwango cha timu na wachezaji, ingawa Kaimu Katibu wa klabu, Baraka Deusdedit alisema jana kwamba hadi sasa wana imani na Pluijm.
    Habari zaidi zinasema Pluijm amekuwa akilalamikiwa hadi na Wasaidizi wake na viongozi wa Kamati ya Mashindano kwamba hataki ushauri. Pluijm pia analalamikiwa kushauri wachezaji ambao wanaonekana bado kuhitajika katika timu kama Salum Telela waachwe na kupendekeza kusajiliwa kwa wachezaji ambao mwishowe hawatumii kama Obrey Chirwa.
    Pluijm alisaini Mkataba mpya wa miaka miwili Julai mwaka huu baada ta kuiwezesha timu kushinda mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
    Hata hivyo, Pluijm aliyeiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola, kuanzia hapo akashindwa kuendeleza matokeo mazuri kwenye mechi za timu hiyo.
    Yanga ilifungwa mechi nne kati ya sita za Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika. 
    Ilifungwa na mbili za TP Mazembe 1-0 Dar es Salaam, 3-1 Lubumbashi, ikafungwa 3-1 na Medeama SC Ghana na 1-0 na MO Bejaia mjini Bejaia, Algria, wakati yenyewe ilishinda mchezo mmoja tu dhidi Bejaia 1-0 Dar es Salaam na kutoa sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam.
    Ikumbukwe Pluijm alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza mwaka 2014, akirithi mikoba ya Mholanzi mwenzake Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, lakini mwisho wa msimu Juni akaondoka kwenda Al Shoalah FC ya Saudi Arabia pamoja na aliyekuwa Msaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa.
    Yanga SC ikamuajiri Mbrazil Maximo, ambaye baada ya miezi mitano akafukuzwa kufuatia kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Simba SC Desemba 13, 2014 na Pluijm akarejeshwa kazini hadi sasa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKWASA: KURUDI YANGA POA TU, WAMALIZANE NA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top