• HABARI MPYA

    Sunday, October 16, 2016

    MANJI ASIFIKIRI WATU WAMO NDANI YA FIKRA ZAKE

    JANA Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji alikutana na viongozi wa Matawi ya Dar es Salaam katika kikao cha siri makao makuu ya klabu, Jangwani.
    Lakini inadaiwa alisema kuna upotoshaji mkubwa katika dhana yake ya kuikodisha klabu na kwamba katika Mkutano wa Oktoba 23 atakuwa tayari kusitisha mpango huo, iwapo atatokea wa kutoa hoja ya kupinga na wanachama wakakubali.
    Nani asiyejua kwamba Manji hawezi kushindwa kwa lolote mbele ya wanachama wa Yanga kwa sasa, kwa sababu amewaweka kwenye kiganja cha mkono wake. 
    Wanachama wa Yanga wanapenda kusikia wachezaji wa kigeni wanasajiliwa kwa mbwembwe na timu yao inashinda. Basi.
    Hawajali kuhusu uwepo wa klabu kesho – na ndiyo maana wamekubali Manji akodishwe timu bila kutaka kujua chochote.
    Na ndiyo maana yeyote anayehoji kwa sasa kuhusu aina ya ukodishaji wa timu wa Manji anaonekana adui tu – hapa suala la mustakabali wa klabu si muhimu tena, bali ni Yanga iendelee kuwa ya Manji.
    Haishangazi leo wana Yanga wanashindwa hata kujiuliza deni la Bilioni 11.6 ambazo klabu hiyo inadaiwa na Manji limetokana na nini.
    Tangu mwaka 2006 Manji amekuwa mfadhili wa Yanga na baadaye Mwenyekiti tangu mwaka 2012 – je hili deni la Bilioni 11.6 ambalo linafanya klabu ikodishwe bure limetokana na nini?
    Lakini hata ukihoji sasa huwezi kueleweka, kwa sababu asilimia kubwa ya wana Yanga hawataki kujua juu ya hilo wao wanataka Manji tu. 
    Ukirudi kwenye historia ya klabu, Manji si mfadhili wa kwanza. Wamepita wengi, akiwemo Abbas Gulamali (marehemu) aliibuka mwaka 1991 na hadi mwaka 2000 alikuwa bado anaisaidia klabu hiyo kabla ya kufikwa na umauti. 
    Gulamali alikarabati hadi jengo. Aliajiri makocha na kusajili wachezaji na kuwalipa pia. Ila, wakati wa kuondoka hakusema anadai chochote. Manji anaikodi timu akiwa anaidai Bilioni 11. 6.
    Je, kama Manji anaidai klabu Bilioni 11.6 tuelewe vipi katika kipindi chake cha kuwa klabu hiyo alikuwa mfadhili au mkopeshaji? 
    Na kama alikuwa mkopeshaji, ni Mkutano upi wa wanachama uliuidhinishia uongozi upi wa Yanga kwenda kukopa hadi deni kufika Bilioni 11.6?
    Tuamini Bilioni 11.6 ni pamoja na fedha zilizotumika kulipa mikataba ya waajiriwa mbalimbali iliyovunjwa kinyume cha utaratibu wakiwemo, makocha, wachezaji na hata viongozi.
    Fedha hizo zinahusu matumizi mbalimbali ya kifahari ya klabu kama kambi za Uturuki, kufukuza na kuajiri makocha ovyo kusajili wachezaji wabovu kwa fedha nyingi na kuwavunjia mkataba baada ya muda mfupi na kadhalika. Zote ni sehemu ya Bilioni 11.6 kuanzia wakati wa Mcameroon Jama Robert Mba hadi Issoufou Boubacar wa Niger.
    Wakati bado hatujapata majibu ya haya – tunazidi kujiuliza zaidi mustakabali wa klabu baada ya kukodishwa na mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Kiasia.
    Binafsi sikatai mabadiliko – bali siko tayari kuunga mkono mabadiliko ya kinyonyaji iwe Yanga hata Simba.
    Hizi klabu hazikuibuka tu, ziliasisiwa na watu waliopoteza muda, nguvu na mali zao kuhakikisha zinasimama na wakazijengea ustawi wa kuwa klabu zenye mvuto hata leo Manji amevutiwa na Yanga. 
    Kama suala ni Manji kukodi tu timu ya Ligi Kuu kwa nini asingekwenda kuikodi Mbao FC au Ndanda – au akaamua tu moja kwa moja kuanzisha timu yake moja kwa moja.  
    Alichokifuata Yanga ndiyo sababu ya watu kuhoji uhalali wake, aina ya mchakato na taratibu za ukodishwaji wake.
    Tatizo linalojitokeza hapa Yanga inakodishwa kama haijui bidhaa zake wala thamani yake baada ya maamuzi kuchukuliwa kwenye mkutano wa dharula ambao watu walimzomea kila aliyetaka ufafanuzi wa kina juu ya suala hilo.
    Mkataba uliovujishwa kwenye vyombo habari hauelezi chochote cha maana zaidi ya vipengele vya kawaida mno na rahisi kama mtu anapanga, au kupangishwa chumba cha kuishi. 
    Mkataba hauelezi hata iwapo Manji ataanzisha biashara baada ya miaka 10 zitabaki kuwa za Yanga, au za kwake, au ataiacha klabu katika hadhi yake ya sasa. 
    Amesema kama kutakuwa na hasara ataibeba na wakati huo huo anasema asilimia 25 ya faida itatumika kujenga Uwanja wa timu – wakati mwezi uliopita alikwenda kuwaonyesha watu eneo Geza Ulole ambalo ataijengea klabu Uwanja na kituo cha soka ya vijana.
    Huyu ni mtu ambaye alikuwa anajinasibu ana mpango wa kuijengea Yanga Uwanja wa kisasa Jangwani, lakini akadai anakwamishwa na Halmashauri ya Jiji.
    Mikanganyiko kama hii wana Yanga hawajali na wanaweza wakakupiga hata mawe kwa kuhoji – wao wanataka Manji tu na hiyo ni kwa sababu hawana uchungu na klabu. 
    Manji aache kufikiria kwamba kuna mtu yumo ndani ya fikra zake juu ya Yanga badala yake awaambie watu anafikiria nini kuhusu klabu hiyo.
    Hakuna anayeweza kupinga mabadiliko katika dunia ya leo – lakini yawe mabadiliko ambayo yataifanya Yanga iendelee kuwa mali ya wana Yanga, bali kuna mtu mwenye sauti na mamlaka zaidi ya wengine kwa sababu ya mchango wake kama ilivyo familia ya Glazier pale Manchester United ya England.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANJI ASIFIKIRI WATU WAMO NDANI YA FIKRA ZAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top