• HABARI MPYA

    Tuesday, October 18, 2016

    MAMILIONI YA SIMBA NA YANGA YASHIKILIWA CELCOM

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KAMPUNI ya Celcom Tanzania Limited inashikilia zaidi ya Sh. Milioni 130 za mapato ya mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Oktoba 1, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hiyo ni baada ya kuondolewa kwa makato mengine yote muhimu kwenye mapato ya jumla ya mchezo huo ulioingiza Sh. Milioni 320 Simba na Yanga zikitoa sare ya 1-1.
    Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE imezipata zinasema kwamba, fedha hizo zimezuiwa kwa maelekezo ya Serikali kufuatia uharibifu uliojitokeza katika mchezo huo wa Oktoba 1, mwaka huu mashabiki wa Simba wakivunja viti.
    Kipa wa Simba, Vincent Angban akijivuta kupigampira mbele ya mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe (kulia)

    Na taarifa zinasema kwamba Serikali imezuia fedha hizo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika juu ya hasara iliyojitokeza, ambayo kimsingi Simba wamekubali kulipa.
    Habari zinasema mchezo huo uliingiza Sh. Milioni 320 wakati uharibifu uliofanywa na Simba unakaribia kuwa wa Sh Milioni 400.
    Makato ambayo yamekwishaondolewa kwenye mapato hayo ni pamoja na asilimia18 ya VAT, asilimia 15 ya gharama za Uwanja, asilima 9 ya Bodi ya Ligi, asilimia 5 ya TFF, asilimia 3 ya DRFA na asilimia 8 ya gharama za mchezo.
    Wenyeji Yanga SC wanastahili kupewa asilimia 40 ya mapato hayo wakati asilimia 20 ni za waliokuwa wageni, Simba SC. 
    Tayari Simba SC wameandika barua TFF kuomba wapatiwe mgawo wao wa mchezo huo kwa kuwa wanahitaki fedha za kujiendesha kwa wakati huu na deni hilo watalipa taratibu.
    Hatua hiyo inakuja kufuatia mashabiki wa Simba kufanya vurugu Uwanja wa Taifa Oktoba 1, baada ya Yanga kupata bao la kuongoza dakika ya 26 lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Kwa hali hiyo, mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya. Lakini tayari TFF imeipiga Simba SC faini ya Sh. Milioni 5 kwa kosa hilo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAMILIONI YA SIMBA NA YANGA YASHIKILIWA CELCOM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top