• HABARI MPYA

  Sunday, October 02, 2016

  KILA LA HERI SERENGETI BOYS LEO KONGO

  Na Mwandishi Wetu, BRAZZAVILLE
  TIMU ya taiufa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys inatarajiwa kushuka dimbani, Uwanja wa Kumbukumbu ya Alphonse Massamba-Debat mjini Brazaville, kumenyana na wenyeji Kongo – Brazzaville katika mchezo wa marudiano hatua ya mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya fainali za U-17 mwakani Madagascar.  
  Serengeti Boys iliyowasili mjini Brazaville Alhamisi ikitokea Kigali, Rwanda ilipoweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo huo wa marudiano, itahitaji hata sare ili kufuzu fainali za U-17 Madagascar baada ya awali kushinda 3-2 nyumbani Dar es Salaam Jumapili wiki iliyopita.
  Wachezaji wa Serengeti Boys iliyo chini Mkurugenzi wa Ufundi, Mdenmark Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime na Kocha wa makipa na Muharami Mohammed ‘Shilton’ wameonekana wenye ari nzuri kuelekea mchezo wa leo.
  Kwa upande wake, kocha Shime anatarajia matokeo mazuri leo baada ya maandalizi mazuri; “Timu iko vizuri. Tumejiandaa vizuri kwa yale ya msingi yote tumekamilisha,”alisema.
  Shime alisema watatumia mfumo wa 4-4-2 katika mchezo wa leo kwa sababu ni rafiki kwa Serengeti Boys kwani wamekuwa wakiutumia katika michezo takribani 15 ya kimataifa hajapoteza hata mmoja, “Kwa hivyo siwezi kubadili mfumo huu. Ni mfumo wa kushambulia na kulinda tusifungwe. Vijana wanauelewa zaidi na ndio mfumo wetu.” 
  Tanzania haijawahi kufuzu fainali zoozote za vijana Afrika – ingawa mwaka 2005 Serengeti Boys ilifuzu fainali za Gambia, kwa kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabawe, lakini ikaenguliwa kwa kashfa ya kumtumia mchezaji aliyezidi umri, Nurdin Bakari aliyekuwa anachezea Simba SC wakati huo.
  Lakini utaratibu mzuri uliotumika kuunda timu ya sasa kwa kufuatilia tarehe halisi ya kuzaliwa kwa mchezaji, inaaminika unaweza kuiepusha Serengeti na majanga kama ya 2005. Kila la heri Serengeti Boys. Mungu ibariki Tanzania.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA LA HERI SERENGETI BOYS LEO KONGO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top