• HABARI MPYA

  Wednesday, October 12, 2016

  AMBAVYO YANGA WAMECHEMKA KUJIKODISHA KWA YANGA YETU!

  HATIMAYE Yanga SC imeingia katika historia mpya kufuatia Baraza la Wadhamini la klabu kuikodisha timu ya soka kwa Kampuni ya Yanga Yetu Limited.
  Yanga Yetu Limited ni kampuni iliyosajiliwa na Mwenyekiti wa Yanga SC, Yussuf Manji ambaye kwa muda mrefu amekuwa akifahamika kama mfadhili pia.
  Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mfadhili awali akitumia kampuni ya Loto Kitita kuidhamini klabu hiyo, wakati huo Mwenyekiti wa klabu akiwa Francis Kifukwe.
  Akasaidia kusuluhisha mgogoro uliokuwapo wa Yanga Kampuni na Yanga Asili kwa gharama kubwa na aliyekuwa mpinzani mkubwa wa uongozi, Mzee Yussuf Mzimba akakubali kukaa kando. Yanga SC yenye umoja bila makundi ikaanza maisha mapya na Wakili Imani Mahugila Madega akachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa klabu baada ya mwafaka.
  Na huo ndiyo wakati ambao Manji alianza kuiyumbisha Yanga kwa kuzozana na Mwenyekiti Madega kutokana na kutaka kuingilia mambo ya uongozi akiwa mfadhili.
  Wazi ugomvi na Manji ulimuathiri mno Madega katika utawala wake Yanga, lakini akapambana akamaliza muda wake na kuitisha uchaguzi mwingine.
  Ilionekana wazi katika uchaguzi huo, Manji alitaka Francis Kifukwe ndiye ashinde, lakini aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Ridhiwani Kikwete alisimama kidete kuhakikisha Mwenyekiti huyo wa zamani harejei madarakani.
  Wakili Lloyd Baharagu Nchunga akashinda uchaguzi kiulaini baada ya Kifukwe kujitoa kufuatia kujiridhisha Kamati ya Uchaguzi chini ya mtoto wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete haimtaki.
  Nchunga akavivaa sawia viatu vya Madega na mwisho wa siku naye kwa misimamo yake akageuka adui wa Manji. Na kwa sababu ya kumeguka kwa Kamati yake ya Utendaji, ikiwemo kuondoka kwa aliyekuwa Makamu wake Mwenyekiti, Davis Mosha, Nchunga akashindwa kupambana na Manji, mwishowe akajiuzulu.
  Ukaitishwa uchaguzi mdogo na Manji akagombea mwenyewe Uenyekiti baada ya kushindwa kufanikisha mipango yake chini ya Mawakili wawili, Madega na Nchunga.
  Baada ya kuingia madarakani, Manji akaanza kutengeneza mazingira ya timu ambayo haitampinga kwa lolote. Akaunda Baraza jipya la Wadhamini, ambalo Kikatiba ndilo huwa wamiliki wa klabu.
  Akagombea katika uchaguzi Mkuu katikati ya mwaka huu baada ya kumaliza muda wake wa uchaguzi mdogo na kufanikiwa kuingia tena madarakani.
  Alipoingia tu madarakani akafanikiwa kuwaondoa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliokataa kuburuzwa naye, ambao ni Inspekta wa jeshi la Polisi Hashim Abdallah na mfanyabiashara Salum Mkemi.
  Bila ya kutazama uhalali wa Baraza hilo la Wadhamini, ambalo halikuidhinishwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa mujibu wa Sheria, lakini sasa linamkodisha timu Manji.
  Kumkodisha Manji timu ni suala moja – lakini Baraza limemruhusu Manji kusajili Kampuni inayoitwa Yanga Yetu Limited ambayo ndiyo imeikodi klabu.
  Kabla hatujaelekea kujadili Mkataba wenyewe wa ukodishwaji wa timu – tunakutana na ukakasi mzito katika hili la Yanga Yetu kuikodi Yanga SC.
  Na Baraza la Wadhamini linatuambia lilipata ushauri wa kisheria kutoka kwa magwiji wa sheria nchini kama Profesa Mgongo Fimbo, Jaji John Mkwawa na Wakili Alex Mgongolwa – inaniwia vigumu mno kuamini hapa.
  Hakuna kitu ambacho ni cha kujivunia kwa klabu hiyo kuliko jina Yanga – hilo thamani yake ni zaidi ya majengo na rasilimali zote ilizonazo. Yanga ndiyo mtaji mkubwa zaidi wa klabu, ambao inasikitisha kwa miaka 80 na zaidi haujatumika ipasavyo.
  Hilo Baraza la Wadhamini lenyewe la Yanga lina watu weledi tu kama akina Kifukwe, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika na Mama Fatuma Karume ambaye ni mke wa Rais wa zamani Zanzibar.
  Lakini ajabu wamethubutu kuruhusu Manji asajili kampuni inaitwa Yanga Yetu, ambayo ndiyo imeikodi klabu ya Yanga.
  Ama kwa hakika watu wa dunia ya leo wamekosa woga kabisa kiasi cha kufikia kufanya maamuzi ya hatari kama haya.
  Kwa nini Manji asisajili kampuni kwa jina lolote, lakini si Yanga (Yetu) ndiyo ikaikodisha Yanga SC.
  Kwa nini Baraza tata la Wadhamini limeruhusu hali hiyo? Sitaki kufikiria kwa nini Manji akodishwe timu bure baada ya uwekezaji mzito uliofanywa tangu miaka ya 1920 na waasisi wa klabu, tu nastaajabu Yanga Yetu kuikodi Yanga SC.
  Na kila anayehoji mapungufu haya, anaonekana hataki mabadiliko – kwa nini sasa Baraza la Wadhamini lisikiri limefanya makosa na mchakato ukaanza upya?
  Kunako majaaliwa, Jumapili nitajadili kuhusu Manji kuidai Yanga Bilioni 11.6 katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na baadaye Mwenyekiti.
  Je, kama Manji anaidai klabu Bilioni 11.6, alikuwa mfadhili au mkopeshaji? Na kama alikuwa mkopeshaji, ni Mkutano upi wa wanachama uliuidhinishia uongozi upi wa Yanga kwenda kukopa hadi deni kufika Bilioni 11.6? 
  Kwa hayo na mengine mengi kuhusu deni hilo na kile kinachoonekana kuwa mpango wa muda mrefu wa Manji siku moja kujimilikisha Yanga kijanja, tuombeane uzima Jumapili inshaalah. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AMBAVYO YANGA WAMECHEMKA KUJIKODISHA KWA YANGA YETU! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top