• HABARI MPYA

    Sunday, September 04, 2016

    YANGA YASAKA KIUNGO WA ULINZI MWENYE SIFA ZA KANTE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Yanga, Hans van der Pluijm anasaka kiungo wa ulinzi mwenye sifa za Mfaransa anayechezea Chelsea ya England, N’Golo Kante amuongeze katika kikosi chake.
    Mholanzi huyo kwa sasa anatupia macho sehemu tofauti kuangalia uwezekano wa kumpata mchezaji mwenye sifa za 
    Kante, kiungo mwenye asili ya Mali aliyekaribia kuipa Ufaransa taji la Euro mwezi uliopita.
    Na Pluijm anaweza hata kumuondoa katika usajili mmoja kati ya wachezaji wake saba wa kigeni, Mbuyu Twite, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Obrey Chirwa, Donald Ngoma au Amissi Tambwe ili asajii mchezaji mwenye sifa za Kante.
    Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm (kushoto) akiwa na Msaidizi wake, Juma Mwambusi
    Mjumbe mmoja wa Kamati ya Mashindano ya Yanga inayohusika na usajili pia aliiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana kwamba Pluijm amegundua timu inakosa kiungo wa ulinzi baada ya wachezaji wote waliopo kushindwa kumudu kucheza nafasi hiyo.
    Na iwapo atapatikana kiungo mzuri wa kigeni wa ulinzi, kuna uwezekano Pluijm akawashitua wengi kwa kumuondoa kwenye usajili mmoja wa wachezaji nyota wa kigeni kwenye timu kwa sasa.
    Diriha la usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linatarajiwa kufungwa Julai 7 na Yanga wana nafasi ya kufanya marekebisho ya usajili wake ndani ya siku mbili hizi.
    Kikosi cha Yanga cha sasa kinaundwa na makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Beno Kakolanya, Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Juma Abdul, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji Mngwali, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Pato Ngonyani, Andrew Vincent ‘Dante’ na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
    Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Simon Msuva, Deus Kaseke, Geoffrey Mwashiuya, Obrey Chirwa na Yussuf Mhilu wakati washambuliaji ni Donald Ngoma, Malimi Busungu, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.  
    Ukiacha Makapu, viungo wengine wote wa Yanga ni wa ushambuliaji kiasili, hali inayowafanya mabingwa hao mara 25 wa Tanzania Bara kuwa na upungufu mkubwa katika eneo hilo muhimu katika kuwalinda mabeki wanne.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YASAKA KIUNGO WA ULINZI MWENYE SIFA ZA KANTE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top