• HABARI MPYA

  Monday, September 19, 2016

  WAWA MGUU NJE AZAM FC, WAARABU WAPANIA KUMNG'OA CHAMAZI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BEKI hodari wa kati Serges Pascal Wawa Sfondo kutoka Ivory Coast, amesema kwamba klabu tatu zimemletea ofa ikiwemo moja ya Tanzania wakati anamaliza Mkataba wake miezi miwili ijayo Azam FC.
  Wawa aliyezaliwa Januari 1, mwaka 1986 mjini Bingerville, Ivory Coast alijiunga na Azam FC mwaka 2014 kutoka El Merreikh ya Sudan, ambayo nayo ilimtoa ASEC Mimosa ya kwao, Ivory Coast mwaka 2010.
  “Ninamaliza mkataba wangu hapa baada ya miezi miwili na hadi sasa sijasaini mkataba mpya. Nina ofa tatu, moja ni Qatar, nyingine ni ya klabu ya hapa hapa Tanzania na nyingine ni El Merreikh wanataka nirudi,”alisema jana Dar es Salaam Wawa akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE.
  Serges Pascal Wawa Sfondo, amesema haelewi mustakabali wake miezi miwili ijayo baada ya kumaliza mkataba wake na klabu hiyo.

  Alipoulizwa kuhusu Azam FC, Wawa aliyeanza kuchezea ASEC mwaka 2003, alisema kwamba hayajafanyika mazungumzo hadi sasa, lakini anaamini anathaminika kwenye timu.
  “Nimekuwa majeruhi kwa muda mrefu, na niliumia nikiwa mchezaji muhimu kwenye timu. Klabu imenitibu na kunihudumia vizuri tangu hapo. Nafurahia kuwepo kwangu Azam, sina tatizo. Lakini haiondoi ukweli sijajua mustakabali wangu,”alisema.
  Ingawa hajaweka wazi sababu za kusema hauelewi mustakabali wake, lakini inaonekana Wawa anataka kutazama mwelekeo wake chini ya makocha wapya kutoka Hispania kabla ya kuamua kujitia pingu nyingine Azam.
  Kwa kipindi chote tangu asajiliwe Azam FC, Wawa amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza akicheza pamoja na ama Aggrey Morris, David Mwantika au Said Mourad aliyeachwa msimu huu – lakini sasa klabu imeleta beki mwingine, Daniel Amoah kutoka Ghana.  
  Na klabu pia ipo chini ya benchi jipya la Ufundi, linaloundwa na makocha kutoka Hispania watupu ambao ni; Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Msaidizi wake Yeray Romero, Kocha Mkuu wa Viungo Jonas Garcia, Msaidizi wake, Pablo Borges, kocha wa Makipa Jose Garcia na Daktari Sergio Perez.
  Jopo hilo la makocha linaongezewa nguvu na wazawa watatu, Kocha Msaidizi Dennis Kitambi na wa Makipa, Idd Abubakar na Meneja Philipo Alando.
  Msimu uliopita Azam FC ilikuwa chini ya kocha Muingereza, Stewart John Hall – lakini Wawa alisajiliwa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog ambaye kwa sasa yupo Simba SC.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAWA MGUU NJE AZAM FC, WAARABU WAPANIA KUMNG'OA CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top