• HABARI MPYA

    Wednesday, September 14, 2016

    WASIOWEZA WAKAE PEMBENI, WAWAPISHE WENGINE WAJARIBU

    HIVI karibuni msafara wa timu ya taifa ya Olimpiki ulirejea mikono mitupu kutoka Rio, Brazil kwenye mashindano ya mwaka huu.
    Jirani zetu Kenya, Uganda, Rwanda na hata Burundi walikuwa wana cha kujivujia baada ya Michezo ya Olimpiki mwaka huu.
    Timu ya taifa ya soka imeshika mkia katika Kundi G kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, nyuma ya Nigeria iliyomaliza nafasi ya pili na Misri iliyoongoza kundi hilo na kufuzu michezo hiyo ya Gabon mwakani.
    Awali timu hiyo ilitolewa na Algeria mwaka jana katika mechi za kuwania tiketi ya kucheza Kombe la Dunia mwaka jana.
    Mabingwa wa soka Tanzania, Yanga SC wameshika mkia katika Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika, nyuma ya Medeama SC ya Ghana, MO Bejaia ya Algeria na TP Mazembe ya DRC. Mazembe na Bejaia zimefuzu Nusu Fainali.
    Azam FC ilitolewa mapema tu katika michuano ya Kombe la Shirikisho hatua za awali.
    Yanga ilianzia Ligi ya Mabingwa Afrika, ambako ilipotolewa hatua ya mwisho ya mchujo wa kwenda kwenye makundi, ikaangukia kwenye mchujo wa kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
    Timu ya taifa ya soka la Ufukweni imetolewa na Ivory Coast katika mechi ya kuwania tiketi ya Fainali za Afrika baadaye mwaka huu Nigeria.
    Timu ya taifa ya soka ya vijana chini ya umri wa 17, Serengeti Boys ndiyo pekee ambayo Watanzania wanapenda kusikia habari zake kwa sasa, baada ya kufanikiwa kufika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya fainali za Afrika mwakani Madagascar, ambako itamenyana na Kongo- Brazaville mwezi huu.
    Mabondia wetu wanaopelekwa na Emannuel Mlundwa kupigana Asia na Ulaya wanapigwa kila wakienda.
    Hali ni mbaya katika sekta ya michezo Tanzania na bahati mbaya moja ya changamoto kubwa ni Serikali ya nchi yetu kutokuwa na mchango wowote kwenye sekta hiyo kwa sasa.
    Hata viongozi wa vyama na mashirikisho mbalimbali ya michezo nchini wamekuwa wana majibu mepesi tu wanaposhutumiwa kushindwa kuleta maendeleo katika michezo wanayoiongoza – kwamba hawapati sapoti ya Serikali.
    Ni kweli nchi za wenzetu zinaweza kwa sababu zinapata sapoti ya Serikali zao, ambazo zinawekeza fedha nyingi.
    Hapa nchini, kila kukicha Serikali inazidi kuipa pigo michezo, kuanzia kufuta michezo ya mashuleni ambayo ilikuwa chimbuko zuri la kuibua vipaji kuanzia baada ya Uhuru hadi miaka ya 1990 hata tukafanikiwa kuwa na wanamichezo hodari walioiletea sifa nchi yetu.
    Hali ni mbaya na huo ndiyo ukweli – ni vigumu kufanya programu za maendeleo ya michezo bila msaada wa Serikali, lakini bahati mbaya Tanzania imekuwa hivyo.
    Pamoja na ukweli huo, bado haitoshi kuwa sababu kwa viongozi wa michezo nchini kila siku kusema wanashindwa kwa sababu hawana sapoti ya Serikali.
    Wakati wanasema hivyo, bado wameendelea kurudia kuomba ridhaa ya kuongoza mchezo ambao wamekwishashindwa kuundeleza kwa sababu inayoingia tu akilini, kukosa sapoti ya Serikali.
    Nadhani sasa imetosha kusema kushindwa kuleta mafanikio kwenye mchezo kunatokana na kukosekana kwa sapoti ya Serikali.
    Watu wanarudi kugombea chama cha mchezo ule ule kila wamalizapo awamu moja, lakini ukihoji maendeleo, jibu linakuwa hakuna sapoti Serikali. Kwa nini wanaendelea kuongoza? Wawapishe wengine, waache kuchezea akili za Watanzania.
    Wakati umefika sasa yeyote anayejitokeza kuwania uongozi kwenye chama au shirikisho lolote la michezo, awe tayari kukabiliana na changmoto pasipo kutoa visingizio – aende kugombea kwa lengo la kuleta maendeleo na visingizio.
    Anayeona hawezi kuleta maendeleo ya michezo kutokana na changamoto zilizopo, asijitokeze kugombea, kuliko kwenda kugombea ili akichaguliwe atoe visingizio vile vile.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WASIOWEZA WAKAE PEMBENI, WAWAPISHE WENGINE WAJARIBU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top