• HABARI MPYA

  Thursday, September 08, 2016

  SARE NA NDANDA JANA, YADAIWA WACHEZAJI YANGA SC WALIKUWA WANA MGOMO BARIDI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KUCHEZA kwa kiwango cha chini jana Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara hadi kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji Ndanda FC kulisababishwa na Yanga SC kutofanya mazoezi kwa siku tatu kuelekea mchezo huo.
  Na imedaiwa timu kutofanya mazoezi kwa siku tatu kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kulisababishwa na mgomo wa wachezaji, jambo ambalo hata hivyo, Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit amekana.
  Imedaiwa wachezaji wa Yanga waligoma wakishinikiza kupewa mishahara yao ya mwezi Julai hadi walipokutana na Mwenyekiti, Yussuf Manji Jumatatu ambaye pia ni mfadhili ndipo wakasitisha mgomo wao.
  Winga wa Yanga, Simon Msuva akipiga krosi pembeni ya beki wa Ndanda, Paul Ngalema

  Yanga ikasafiri Jumanne asubuhi kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo na Ndanda, uliomalizika kwa sare ya 0-0. Na waliingia kwenye mchezo wa jana baada ya mazoezi mepesi tu, tena ya siku moja Uwanja wa Nangwanda.   
  Yanga jana ilicheza kichovu ikilazimishwa sare na Ndanda – na kumbe kilichojificha nyuma ya hali hiyo ni timu kutofanya mazoezi kwa siku tatu.
  Na inadaiwa huo ni mgomo wa pili ndani ya wiki mbili, baada ya awali wachezaji kugoma kuelekea mchezo wa mwisho wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe mjini Lubumbashi, DRC.
  Inadaiwa waligoma kushinikiza kulipwa posho walizoahidiwa na Manji kwa kutwaa mataji matatu (Ligi Kuu, Kombe TFF na Ngao ya Jamii) msimu uliopita, kuwafunga mahasimu Simba mechi zote mbili na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
  Hata hivyo, baadaye timu ilisafiri kwenda Lubumbashi, ambako ilichapwa mabao 3-1. 
  Waliporejea walikutana na Manji – ingawa haijulikani kama walilipwa au la, lakini wakaendelea na majukumu yao katika Ligi Kuu, wakiingia uwanjani katika mchezo wa kwanza na kuifunga African Lyon 3-0.  
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Katibu wa Yanga SC, Baraka Deusdedit kwanza alikana si kweli kwamba wachezaji waligoma, lakini akakiri timu haikufanya mazoezi siku tatu kabla ya mchezo na Ndanda.
  Deusdedit alisema kwamba kilichotokea ni kocha Mholanzi Hans van der Pluijm aliwapa mapumziko wachezaji wikiendi (Jumamosi na Jumapili) na bahati mbaya Jumatatu kukawa na kikao na Mwenyekiti, Manji katika utaratibu wa kawaida wa klabu.
  “Kwa hiyo kama kuna dhana hiyo ya timu kutoa sare jana kwa sababu ya kutofanya mazoezi siku tatu, benchi la Ufundi litasema katika taarifa yake,”alisema Baraka.
  Pamoja na hayo, Baraka akalalamikia Yanga kupangiwa mechi nyingine ya Ligi Kuu Jumamosi dhidi ya Maji Maji, wakati jana wamecheza Mtwara.
  “Sisi tumeondoka leo Mtwara, tutafika Dar es Salaam mchana na hatutafanya mazoezi leo. Kesho ni Ijumaa na keshokutwa Jumamosi tuna mechi nyingine, wakati Simba waliocheza jana Dar es Salaam wana mechi nyingine Jumapili,”alisema.
  Baraka amesema kwamba ingekuwa bora kama Simba ndiyo wangecheza Jumamosi na Yanga wakacheza Jumapili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SARE NA NDANDA JANA, YADAIWA WACHEZAJI YANGA SC WALIKUWA WANA MGOMO BARIDI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top