• HABARI MPYA

  Thursday, September 15, 2016

  SAMATTA AANZA KUKINUKISHA MAKUNDI ULAYA LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BAADA ya kufungwa mabao 2-0 na Standard Liege katika Ligi ya Ubelgiji Jumapili Uwanja wa Maurice Dufrasne mjini Liege, Nahodha wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta leo anatarajiwa kuiongoza tena KRC Genk katika mchezo wa kwanza wa Kundi F Europa League dhidi ya wenyeji, Rapid Viena nchini Austria.
  SK Rapid Wien watakuwa wenyeji wa KRC Genk Uwanja wa Allianz, wakati katika mchezo mwingine wa kundi hilo, 
  Sassuolo ya Italia watakuwa wenyeji wa Athletic Bilbao ya Hispania Uwanja wa Citta del Tricolore.
  Na wakati mechi za makundi zinaanza Europa League,tayari Samatta alisema wamepangwa kundi gumu tofauti na watu wanavyofikiria.
  Mbwana Ally Samatta leo anatarajiwa kuiongoza tena KRC Genk katika mchezo wa kwanza wa Kundi F Europa League dhidi ya wenyeji, Rapid Viena nchini Austria

  “Kundi linaonekana kama rahisi, lakini siyo rahisi, timu zote ni timu zenye uzoefu wa mashindano ya Ulaya, wamekuwa washiriki karibu kila mwaka, kwa hiyo binafsi nategemea kukutana na upinzani mkali katika hatua hiyo ya makundi,”alisema.
  Tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza jumla ya mechi 24 za mashindano yote, 18 msimu uliopita na sita msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.
  Katika mechi hizo, ni 13 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na tatu msimu huu, wakati 11 alitokea benchi nane msimu uliopita na tatu msimu huu – na mechi nane hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na mbili msimu huu.
  Na huu utakuwa mchezo wa pili tangu Samatta arejee Ulaya, akitokea kuichezea timu yake ya taifa, Taifa Stars ikipigwa 1-0 na wenyeji, Nigeria katika mchezo wa mwisho wa Kundi G kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Uyo, Akwa Ibom Jumamosi iliyopita.
  Bao pekee la Super Eagles lilifungwa na mshambuliaji wa Manchester City, Kelechi Iheanacho dakika ya 78 katika mchezo uliokuwa mkali na wa kusisimua. Misri iliyovuna pointi 10, imefuzu kiulaini hususan baada ya Chad kujitoa katika kundi hilo katika ya mechi za kufuzu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AANZA KUKINUKISHA MAKUNDI ULAYA LEO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top