• HABARI MPYA

  Saturday, September 17, 2016

  NI PATASHIKA ILE YA NGUO KUCHANIKA SIMBA NA AZAM LEO TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC  na Simba SC zinakutana jioni ya leo katika vita ya kuwania usukani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam.
  Timu hizo zimebanana kwa pointi hadi wastani wa mabao baada yaa mechi nne za awali za Ligi Kuu, kila moja ikishinda tatu na kutoa sare moja – maana yake mshindi wa mchezo huo atatanua kwapa pale juu. 
  Ni mechi ya kwanza kabisa ya msimu baina ya timu hizo – zote zikiwa chini ya makocha wapya.
  Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon Joseph Marius Omog misimu miwili iliyopita tu alikuwa kocha wa Azam, kabla ya kuondoka kumpisha Muingereza, Stewart Hall, ambaye naye mwishoni mwa msimu uliomalizika aliondoka pia.
  Said Ndemla wa Simba SC akiwatoka viungo wa Azam, Salum Abubakar 'Sure Boy' (kulia) na Jean Baptiste Mugiraneza (kushoto) katika mchezo wa Ligi Kuu msimu uliopita 

  Azam pia ipo chini ya benchi jipya linaloundwa na makocha vijana watupu kutoka Hispania, wakiongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Msaidizi wake Yeray Romero, Kocha Mkuu wa Viungo Jonas Garcia, Msaidizi wake, Pablo Borges, kocha wa Makipa Jose Garcia na Daktari Sergio Perez.
  Jopo hilo la makocha linaongezewa nguvu na wazawa watatu, Kocha Msaidizi Dennis Kitambi na wa Makipa, Idd Abubakar na Meneja Philipo Alando.
  Benchi la Ufundi la Simba, mbali na Omog kuna kocha Msaidizi Mganda, Jackson Mayanja, kocha wa makipa ‘Meja’, Meneja Mussa Hassan Mgosi, Mratibu Abbas na Daktari Yassin Gembe.
  Azam imecheza mechi mbili nje ya nyumbani, mjini Mbeya ambako ilishinda zote, 1-0 dhidi ya Prisons na 2-1 dhidi ya Mbeya City, wakati imekuwa ikicheza Uwanja wa Uhuru.
  Na katika sare zao, zote zimebanwa na timu za mjini, Simna wakidroo na JKT Ruvu 0-0 na Azam wakilazimisha sare ya 1-1 na African Lyon.
  Upande wa Azam, Nahodha John Bocco ‘Adebayor’ anaendelea kuwa kinara wa mabao timu, wakati kwa Simba SC, Ibrahim Hajib na Mrundi Laudit Mavugo ndiyo wametokea kuwa wafungaji wa uhakika wa timu hadi sasa.
  Safu zote za ulinzi zina watu wapya wenye uzoefu mkubwa, Simba wanaye Method Mwanjali kutoka Zimbabwe aliyewahi kuchezea hadi Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini na Azam wanaye Daniel Amoah kutoka Medeama SC ya Ghana.
  Mbali na mchezo huo, mabingwa watetezi; Yanga SC baada ya kuvuna pointi saba katika mechi tatu, moja ikicheza ugenini na kutoa sare ya 0-0 na Ndanda FC, nao leo watakuwa wageni wa Mwadui FC ya kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
  Kutakuwa ni mechi ya mahasimu wa Jiji la Mbeya, kati ya Mbeya City na Prisons Uwanja wa Sokoine na wapinzani wa kutengeneza sukari, kati ya Mtibwa Sugar na Kagera Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu; Ruvu Shooting na Mbao FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani na Maji Maji na Ndanda FC Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
  Jumapili kutakuwa na michezo miwili, Stand United wakiikaribisha JKT Ruvu Stars Uwanja wa Kambarage, Shinyanga wakatio Jumanne African Lyon watamenyana na Toto Africans Uwanja wa Uhuru.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI PATASHIKA ILE YA NGUO KUCHANIKA SIMBA NA AZAM LEO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top