• HABARI MPYA

  Wednesday, September 07, 2016

  NDANDA WAIHENYESHA YANGA NANGWANDA, SARE 0-0

  Na Princess Asia, MTWARA
  YANGA SC imelazimishwa sare ya bila kufungana na Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hanse Mabena wa Tanga aliyesaidiwa na Nicholas Makaranga wa Morogoro na Hajji Mwalukuta wa Tanga, Ndanda itabidi wajilaumu kwa kushindwa kupata bao, licha ya kuwazidi kimchezo Yanga.
  Ndanda waliutumia vizuri Uwanja wa nyumbani kwa kutawala tu mchezo, lakini wakashindwa kumfunga kipa mzoefu wa mabingwa watetezi, Ally Mustafa ‘Barthez’.
  Sifa zaidi zimuendee beki mpya chipukizi, Andrew Vincent ‘Dante’ aliyeua mashambulizi mengi ya hatari ya Ndanda pamoja na kuokoa mpira mmoja uliokuwa unaelekea nyavuni kufuatia shuti la Omary Mponda.
  Kipa wa Ndanda Jeremiah Kisubi akidaka mpira mbele ya Obrey Chirwa wa Yanga leo
  Nahodha wa Ndanda, Kiggi Makassy akipambana na winga wa Yanga, Simon Msuva huku wachezaji wengine wakishuhudia
  Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma akiwatoka mabeki wa Ndanda
  Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akipasua katikati ya wachezaji wa Ndanda
  Kiungo mpya mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa alipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 25 baada ya kupewa pasi nzuri na mshambuliaji mwenzake wa zamani wa FC Platinum ya Zimbabwe, Donald Ngoma.
  Mzimbabwe Ngoma na winga wa Taifa Stars, Simon Msuva wote baadaye wakapoteza nafasi nzuri za kufunga. 
  Yanga kidogo ilianza kucheza vizuri kwa mwelekeo wa kutafuta bao dakika 20 za mwisho, wachezaji wake wakigongena vizuri pasi, lakini safu ya ulinzi ya Ndanda iliyoongozwa na Salvatory Ntebe ilisimama imara kutimua mipango yote.
  Yanga ilipoteza nafasi nyingine nzuri ya kupata bao dakika ya 90 na ushei baada ya kupata mpira wa adhabu wa kupiga ndani ya boksi, kufuatia kipa wa Ndanda Jeremiah Kisubi kudaka mpira, kudunda na kutembea nao.
  Wachezaji wa Yanga walilaumiana wenyewe kwa wenyewe baada ya mchezo ambao walikuwa wana matumaini makubwa ya ushindi.
  Yanga inakamilisha michezo miwili ya Ligi Kuu, ikitimiza pointi nne, baada ya kushinda 3-0 mechi ya kwanza dhidi ya African Lyon, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam  wiki iliyopita. 
  Michezo mingine ya Ligi Kuu leo, Simba SC imeshinda 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, wakati bao pelee la Muivory Coast, Kipre Balou limeipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
  Kikosi cha kilikuwa Ndanda FC; Jeremiah Kisubi, Bakari Mtama, Paul Ngalema, Hemed khoja, Salvatiry Ntebe, Ibrahim Isihaka, Salum Minely/Nassor Kapama dk66, Salum Telela, Omary Mponda, Shijja Mkinna na Kiggy Makassy.
  Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Andrew Vincent ‘Dante’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Deus Kaseke/Juma Mahadhi dk58, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Obrey Chirwa
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDANDA WAIHENYESHA YANGA NANGWANDA, SARE 0-0 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top