• HABARI MPYA

    Thursday, September 15, 2016

    MRISHO NGASSA ATIMKIA UMANGANI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa ameondoka leo Dar es Salaam kwenda Muscat, Oman kwa ajili ya mazungumzo na klabu mbili, ikiwemo Fanja. 
    Ngassa, mchezaji huyo wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba, Yanga SC, Azam FC na Simba za Dar es Salaam anakwenda Oman, kiasi cha wiki mbili tangu avunje mkataba na klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo saa chache kabla ya kuondoka, Ngassa alisema; "NInakwenda kufanya mazungumzo na Fanja,"alisema.
    Mrisho Ngassa (kushoto) akimtoka mchezaji wa timu pinzani katika moja ya mechi za Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini
    "Nimekuwa na mazungumzo nao ya awali, tukafikia pazuri tu, sasa wamenitumia tiketi ninakwenda kuzungumza nao," alisema Ngassa moja ya sababu alizotaja wakati anaondoka Free State alisema ni timu ambayo haina malengo ya kushinda taji.
    Ngassa alijiunga na Free State Stars Mei mwaka jana akisajiliwa na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri kwa mkataba wa miaka minne.
    Hata hivyo, kocha aliyemsajili baba huyo wa Farida (9) na Faria (7) alifukuzwa baada ya miezi miwili tu.
    Katika kipindi cha mwaka mmoja wa kuwa Free State, Ngassa amefanya kazi na makocha wanne akiwemo huyu wa sasa, Mfaransa Denis Lavagne aliyeanza kazi Juni mwaka huu.
    Wengine ni Mjerumani Ernst Middendorp aliyefanya kazi kati ya Septemba na Desemba 2015, Mtaliano Giovanni Solinas aliyefanya kazi kati ya Desemba na Mei 2016.
    Na Lavagne ndiye aliyechangia Ngassa kuomba kuondoka Free State baada ya kuonyesha kuidharau Tanzania haiwezi kuwa na mchezaji bora.
    Lavagne alimuanzishia benchi Ngassa katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya ABSA ya Afrika Kusini Agosti 23, kabla ya kumuingiza dakika ya 63 kwenda kuchukua nafasi ya Mbuyiselo Thethani wakati huo tayari FS imekwishapigwa 2-1, matokeo yaliyodumu hadi mwisho wa mchezo.
    Na baada ya kuingia Ngassa akaenda kucheza kwa kiwango kizuri na kukaribia kufunga mara mbili hadi kocha huyo akampongeza baada ya mchezo, ingawa tayari mchezaji wa Tanzania alikwishatumbukiwa nyongo na Mfaransa huyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MRISHO NGASSA ATIMKIA UMANGANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top