• HABARI MPYA

    Thursday, September 08, 2016

    KOCHA MSOMALI AFARIKI DUNIA MOROGORO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA maarufu wa zamani nchini, Mohammed Hassan Msomali amefariki dunia mchana wa leo mjini Morogoro.
    Taarifa iliyothibitishwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ni kwamba Msomali aliyewahi kuchezea timu mbalimbali Morogoro, ikiwemo Mseto amefariki dunia leo.
    “Ni kweli Msomali amefariki dunia, na mimi nimepata taarifa hizo leo. Tumezipokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizi, soka ya Tanzania imempoteza gwiji na mtu muhimu sana,”alisema Malinzi.
    Buriani Mohammed Hassan Msomali, soka ya Tanzania imempoteza gwiji na mtu muhimu 

    Msomali alianza kuwika kama mchezaji na alikuwemo katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichoshiriki Michezo ya Afrika mjini Lagos nchini Nigeria mwaka 1973 pamoja na magwiji wengine kama Maulid Dilunga, Omary Mahadhi ambao wote tayari marehemu pia na Abdallah KIbadeni.
    Kocha huyo wa mabingwa wa Tanzania Bara mwaka 1975, Mseto ya Morogoro – aliwahi pia kufundisha timu za taifa za Bara na Muungano, Taifa Stars, akisaidiwa na Mzee Kategile, baba wa winga wa zamani wa Simba, Alfred Kategile kuanzia mwaka 1980 hadi 1983. 
    Msomali atakumbukwa zaidi Morogoro kwa kuibua vipaji vya wachezaji wengi kitaifa, akiwemo Zamoyoni Mogella, aliyemuita timu ya Bara mwaka 1981, licha ya kuonekana mdogo kwa sababu ya umbo lake, lakini akaibuka mfungaji bora wa mashindano.    
    Pamoja na kucheza na kufundisha, Msomali pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Ujumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF miaka minne iliyopita. Kabla ya kifo chake, Msomali alikuwa mmoja wa wakufunzi wa ukocha nchini.
    Buriani. Gwiji wa soka Morogoro na Tanzania, Mohamed Hassan Msomali. Hakika sisi sote ni haki yake kwa Allah tutarejea. Allah akupe kauli thabiti inshaallah. Pumzika kwa amani Msomali.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA MSOMALI AFARIKI DUNIA MOROGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top