• HABARI MPYA

    Wednesday, September 07, 2016

    KANUNI NYINGINE ZINAZIKANDAMIZA, ZINAZIBEBA BAADHI YA TIMU LIGI KUU

    LIGI  na mashindano yote ya ndani vilikwenda mapumzikoni wikiendi hii kupisha kalenda ya kimataifa.
    Barani Ulaya na Amerika kulikuwa kuna mechi za kufuzu Kombe la Dunia sawa na Asia, wakati kulikuwa kuna mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika. 
    Ni Ligi Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara pekee iliendelea mwishoni mwa wiki, lakini baadhi ya mechi ziliahirishwa kwa sababu ya timu kadhaa zilikuwa na wachezaji watano au zaidi katika timu ya taifa, Taifa Stars.
    Mchezo kati ya mabingwa wa Ligi Kuu, Yanga SC dhidi ya JKT Ruvu uliokuwa uchezwe Jumatano ya Agosti 31 haukufanyika kwa sababu siku hiyo ndiyo Taifa Stars iliondoka kwenda Nigeria.
    Na kwa kuwa Yanga iliangukia kwenye mkumbo wa kuwa na wachezaji wengi Taifa Stars, ikanufaika na kusogezewa mbele mchezo wake.
    Lakini zote, Azam, Simba na Yanga hazikucheza Ligi Kuu mwishioni mwa wiki kwa sababu kimazoea hizo ndizo timu zenye mchango wa wachezaji wengi Taifa Stars. 
    Kwa kuwa TFF ilikuwa inafahamu mapema kabla ya kupanga ratiba kwamba wikiendi hiyo kutakuwa na mchezo wa Taifa na Nigeria, haikuzipanga timu hizo kucheza Ligi Kuu.
    Timu nyingine zote zilicheza Ligi mwishoni mwa wiki kuanzia Jumamosi, Kagera Sugar ikaifunga 1-0 Mwadui, Mtibwa Sugar ikashinda ugenini 2-1 dhidi ya Maji Maji mjini Songea, JKT Ruvu ikalazimishwa sare ya 0-0 na African Lyon na Mbao ikachapwa 4-1 nyumbani Mwanza na Mbeya City.
    Hapa kuna kasoro katika kanuni za Ligi Kuu juu ya kipengele cha timu kuahirishiwa mechi iwapo tu itakuwa ina wachezaji watano au zaidi katika timu ya taifa.
    Kanuni hii imepitwa na wakati na ndiyo maana huwezi kuikuta popote duniani, zaidi ya hapa Tanzania. Kote duniani, wakati wa mechi za timu ya taifa Ligi nzima husimama na si kutazama timu ipi ina wachezaji wangapi. Hapana. Mashindano yote ya ndani yanasimama kupisha kalenda ya kimataifa.
    Na ndiyo maana hivi sasa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limeweka utaratibu maalum wa vipindi vya mechi za kirafiki, ili kuepusha mechi holela za kimataifa – na sasa kuna kalenda mechi ya mechi za kirafiki za FIFA.
    Soka ya sasa inazingatia zaidi mfumo, hivyo kukosekana kwa mchezaji mmoja tu kunaweza kuidhoofisha timu. Mfano kutaka Barcelona iendelee kucheza mechi zake kisa ni Lionel Messi pekee kaitwa timu ya taifa, hautaitendea haki klabu na mashabiki wake. 
    Hapa nchini, msimu uliopita Mganda Hamisi Kiiza ndiye alikuwa kila kitu katika safu ya ushambuliaji. Alipokosekana Simba iliyumba. Kama angekuwa ni yeye pekee ameitwa timu ya taifa na ukaitaka Simba iendelee kucheza, usingeitendea haki.
    Mashabiki wengine hulipa viingilio kwenda kumuona mchezaji hulani nyota, lakini anapokosekana wanaweza wasiende kwa kuhofia hawatashinda na hata wachezaji huathirika kisaikolojia kwa kujua kuwa watapata wakati mgumu kushinda kama tegemeo lao hayupo. 
    TFF wanapaswa kutambua kwamba baadhi ya kanuni za Ligi Kuu zinahitaji kuzifanyia marakebisho, mfano hii isemayo timu yenye wachezaji watano timu ya taifa ndiyo itaahirishiwa mechi wakati wa kalenda ya kimataifa imepitwa na wakati na haitendi haki.
    Ligi na mashindano yote ya nyumbani zinapaswa kusimama wakati  wa kalenda ya kimataifa kama ambavyo nchi nyingine zimekuwa zikifanya na si kuchagua mechi kwa idadi hya wachezaji wa timu ya taifa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KANUNI NYINGINE ZINAZIKANDAMIZA, ZINAZIBEBA BAADHI YA TIMU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top