• HABARI MPYA

    Sunday, September 04, 2016

    HAO NDIYO WACHEZAJI WETU NA AKILI ZAO, LAKINI MAJUTO NI MJUKUU

    KATIKA kikosi cha sasa cha Simba SC, kuna mchezaji anaitwa Mwinyi Kazimoto Mwitula.
    Kiungo huyo mkongwe kwa sasa alirejea timu Msimbazi msimu uliopita baada ya zaidi ya msimu mmoja wa kuichezea Al Markhiya ya Qatari.
    Kazimoto aliondoka Qatari alikokuwa analipwa vizuri zaidi akaamua kurejea Simba. Hakufukuzwa. Na hadi anaondoka, ile timu ilikuwa inamlilia abaki. Lakini sasa yuko Simba SC tena na kama anafurahia maisha pale, au tofauti anajua mwenyewe. Ila ameondoka kwenye maslahi na mazingira mazuri zaidi ya kucheza soka na kurudi Simba. 
    Haruna Moshi Shaaban alinunuliwa na
    Gefle IF ya Sweden mwaka 2010, lakini hakudumu klabu hiyo akavunja mkataba na kurejea Simba SC.
    Alicheza Simba kwa miaka miwili baada ya hapo akafukuzwa kwa sababu za utovu wa nidhamu, akaenda Coastal Union na sasa yuko Mbeya City.
    Anakumbuka maisha na maslahi mazuri aliyoyaacha Ulaya na kurejea Simba na kama anajilaumu anajua mwenyewe.
    Lakini hawa ni wa juzi tu, nyuma kabisa miaka ya 1990 wachezaji kadhaa wa Tanzania waliwahi kufanya maamuzi ya kushangaza kama haya.
    Tukio la kukumbukwa zaidi ni la winga Edibily Jonas Lunyamila kuacha kuendelea na mipango ya kupata timu Ujerumani iliyokuwa inaendelea vizuri na kuamua kurejea Yanga.
    Athumani China naye akiwa kijana mdogo wa umri wa miaka 24 aliwahi kuondoka Uingereza akiwa amesajiliwa na timu ya Daraja la Tatu na kurudi nyumbani Tanzania kuendelea na kazi Yanga SC.
    Athumani Iddi ‘Chuji’, Jerry Tegete wote hawa ninakumbuka walikataa ofa za kwenda Sweden wakiwa katika viwango vizuri ili wabaki Yanga, ambako baadaye waliishia kufukuzwa tu na wengine hadi leo wanadai stahiki zao, hawajalipwa.      
    Na jana kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa amerejea nyumbani Tanzania baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.
    Mchezaji huyo wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba, Yanga SC, Azam FC na Simba za Dar es Salaam alivunja mkataba na klabu hiyo Ijumaa mchana na Jumamosi jioni akawa tayari yuko Dar es Salaam.
    Hiyo ilifuatia kikao kirefu na Meneja Mkuu wa Free State Stars, Rants Makoena makao makuu ya klabu, Mtaa wa President Boshoff Bethlehem, Afrika Kusini kujadili masuala mbalimbali kabla ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba.
    “Ngassa alikuwa ana hoja zake kama mchezaji akitaka kuvunja mkataba, baada ya majadiliano marefu, kiungwana tukakubaliana naye. Tunamtakia safari njema, hatuna kinyongo naye,”alisema Mokoeana.
    Habari za ndani zinasema mwezi wote wa Agosti Ngassa amekuwa akishinikiza kuondoka Free State na baada ya uongozi kuhisi hauwezi kumzuia tena ukamleta Hamisi Kiiza, mchezaji mwingine wa zamani wa zamani wa Simba na Yanga ambaye tayari amejiunga na timu hiyo.
    Kwa upande wake, Ngassa alisema kwamba sababu kubwa za kuondoka Free State ni timu ambayo haina malengo ya kushinda taji.
    “Ninapenda kushinda mataji, nimezoea kushinda mataji tangu nipo mdogo, na nina rekodi ya kushinda mataji tangu klabu yangu ya kwanza ya Ligi Kuu (Kagera Sugar). Ninaondoka Free State kwenda kujiunga na klabu ambayo itanirejesha kwenye enzi za kushinda mataji,”alisema Ngassa.
    Alipoulizwa ni timu gani anakwenda baada ya kuondoka Free State Stars, Ngassa alisema; “Utaijua baada ya muda si mrefu,”. 
    Ngassa alijiunga na Free State Stars Mei mwaka jana akisajiliwa na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri kwa mkataba wa miaka minne.
    Hata hivyo, kocha aliyemsajili baba huyo wa Farida (9) na Faria (7) alifukuzwa baada ya miezi miwili tu.
    Katika kipindi cha mwaka mmoja wa kuwa Free State, Ngassa amefanya kazi na makocha wanne akiwemo huyu wa sasa, Mfaransa Denis Lavagne aliyeanza kazi Juni mwaka huu.
    Wengine ni Mjerumani Ernst Middendorp aliyefanya kazi kati ya Septemba na Desemba 2015, Mtaliano Giovanni Solinas aliyefanya kazi kati ya Desemba na Mei 2016.
    Na Lavagne ndiye aliyechangia Ngassa kuomba kuondoka Free State baada ya kuonyesha kuidharau Tanzania haiwezi kuwa na mchezaji bora.
    Lavagne alimuanzishia benchi Ngassa katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya ABSA ya Afrika Kusini Agosti 23, kabla ya kumuingiza dakika ya 63 kwenda kuchukua nafasi ya Mbuyiselo Thethani wakati huo tayari FS imekwishapigwa 2-1, matokeo yaliyodumu hadi mwisho wa mchezo.
    Na baada ya kuingia Ngassa akaenda kucheza kwa kiwango kizuri na kukaribia kufunga mara mbili hadi kocha huyo akampongeza baada ya mchezo, ingawa tayari mchezaji wa Tanzania alikwishatumbukiwa nyongo na Mfaransa huyo.
    Ngassa akazidisha shinikizo la kutaka kuondoka baada ya mchezo huo hatimaye leo amefanikiwa kuachana salama na klabu hiyo, iliyokaribia kuuzwa Julai kutokana na ukata.
    Kuondoka kwa Ngassa Free State kumepokewa kwa mitazamo tofauti na watu mbalimbali nchini, wakiwemo wachambuzi wa masuala ya soka na wanasoka.
    Wengi wanamkandia kijana huyo kwamba huo ni muendelezo wa maamuzi yake ya ajabu tangu anaibuka kisoka nchini, alipokataa ofa za kwenda kucheza Ulaya, baadaye El Merreikh ya Sudan ili acheze Yanga.
    Makosa aliyowahi kuyafanya Ngassa awali – yanafanya mtu yeyote asiwe tayari kumskiliza na hadithi yake ya kuondoka Free State hata kama amefanya maamuzi sahihi.
    Wengi walimponda na wameendelea kumponda Lunyamila kwa maamuzi yake ya kuondoka Ujerumani kurudi Yanga na bila shaka hata yeye anajutia uamuzi huo.
    Wengi walimponda Boban alipoondoka Ulaya kurudi Simba na bila shaka hata yeye kwa sasa anajuta – na kuhusu Kazimoto, kadhalika maamuzi yake yalistaajabisha.
    Lakini hao ndiyo wachezaji wetu na hizo ndizo akili zao, ila majuto ni mjukuu. Karibu tena nyumbani Ngassa.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAO NDIYO WACHEZAJI WETU NA AKILI ZAO, LAKINI MAJUTO NI MJUKUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top