• HABARI MPYA

    Tuesday, September 06, 2016

    AZAM FC: HATUKUJA KUUZA SURA MBEYA, TUMEFUATA POINTI SITA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez Rodriguez amesema kwamba wanataka kubeba pointi zote sita katika mechi zao mbili za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mjini Mbeya.
    Azam FC wanacheza na Prisons kesho Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya katika mfululizo wa Ligi Kuu na Jumamosi watahitimisha mechi zao za mjini humo kwa kumenyana na Mbeya City.
    Na Rodriguez amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa wamekuja na kazi moja tu mkoani Mbeya, kusaka pointi sita wakianza na ushindi kwa mchezo wa kesho dhidi ya maaafande hao.
    Zeben Hernandez Rodriguez (katikati) anataka kubeba pointi zote sita katika mechi zao mbili za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mjini Mbeya

    “Lakini izingatiwe ya kuwa ligi sio nyepesi kiasi hicho kutokana na timu zote tulizocheza nazo kujiandaa, kikubwa tumekuja kufanya kazi tutaonyesha uwezo wetu, lakini tunaamini kuwa tutahakikisha tunapata zile pointi ambazo tumekuja huku kuzifuata na baada ya hapo tutarudi nyumbani (Dar es Salaam) kucheza mchezo dhidi ya Simba,” alisema.
    Baada ya mapumziko ya wiki moja kupisha wiki ya mechi za timu ya Taifa, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, inatarajia kuendeleza kampeni yake ya kutwaa taji la Ligi Kuu.
    Tayari kikosi cha Azam FC kipo kamili tokea juzi Jumapili kilipwasili jijini hapa kwa ajili ya mchezo huo sambamba na ule wa Jumamosi ijayo (Septemba 10) dhidi ya Mbeya City.
    Kwa miaka mingi sasa tokea Azam FC ipande Ligi Kuu Julai 27, 2008, imekuwa ikikutana na upinzani mkali kutoka kwa maafande hao katika mechi zote za nyumbani na ugenini.
    Mara ya kwanza timu hizo zilikutana Oktoba 25, mwaka 2008 Uwanja wa Sokoine na Prisons ikashinda 2-0. Hadi sasa katika rekodi zao, Azam FC na Tanzania Prisons zimekutana mara 12 ndani ya ligi, huku rekodi zao zikifanana kwenye kila kitu kuanzia mechi za kushinda hadi walizotoka sare.
    Rekodi hizo zinaonyesha kuwa, nusu ya mechi hizo 12 (mechi sita) timu hizo zimeenda sare huku pia kila upande ukishinda mara tatu.
    Jumla ya mabao 20 yamefungwa na timu hizo katika mechi zote 12 walizokutana, cha kustaajabisha zaidi kila timu imefunga mabao 10 jambo ambalo linaongeza zaidi mvuto kwenye mchezo wa kesho.
    Hadi timu hizo zinakutana tena, Azam FC imeonekana kuwa na takwimu nzuri ya ufungaji mabao kuliko Prisons msimu huu, wakati wote wakiwa wamecheza mechi mbili mpaka sasa matajiri hao wamefunga manne huku maafande hao wakitupia mawili tu, lakini wote wameruhusu wavu wao kuguswa mara moja.
    Ukiondoa mechi za ligi, pia timu hizo zimewahi kukutana katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) Machi 31 mwaka huu ndani ya Uwanja wa Azam Complex, mchezo ambao uliisha kwa Azam FC kuibuka kidedea kwa kufuzu kwa nusu fainali kwa ushindi wa mabao 3-1, yaliyofungwa na Shomari Kapombe aliyetupia mawili na Khamis Mcha akitupia moja.
    Pambano hili limeonekana kufanana na lile la msimu uliopita kwenye mzunguko wa pili kwa upande wa Azam FC, ambapo matajiri hao wataingia dimbani wakiwa na lengo kubwa la kuibuka na ushindi ili kurejea kileleni katika msimamo wa ligi.
    Vilevile Februari 24 mwaka huu zilipokutana mara ya mwisho ndani ya uwanja huo, Azam FC iliingia dimbani ikiwa na nia ya kuibuka na ushindi ili kurejea kileleni kwa kuishusha Yanga, lakini ilishindwa kufikia malengo hayo kufuatia mchezo kuisha kwa sare ya bila kufungana.
    Hivyo, hata kesho ushindi wowote wa zaidi ya bao moja kwa upande wa Azam FC, utaifanya kurejea kileleni kwenye msimamo ikifikisha pointi saba na kuishusha Mbeya City ambayo nayo ina pointi hizo lakini itazidiwa idadi ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa (GD) kwani mpaka sasa imefunga mabao manne tu na kufungwa moja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC: HATUKUJA KUUZA SURA MBEYA, TUMEFUATA POINTI SITA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top