• HABARI MPYA

  Tuesday, August 02, 2016

  TFF YACHIMBA MKWARA; "HUNA MKATABA, HUCHEZI LIGI KUU"

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limekumbusha kwamba halitatoa leseni kwa mchezaji yeyote wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ambaye hatakuwa na mkataba wakati anaombewa usajili.
  Taarifa ya TFF leo imesema kwamba hiyo ni kwa mujibu wa kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya Tanzania toleo la 2016/2017 kwamba kila timu inatakiwa kuwasilisha nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. 
  Rais wa TFF, Jamal Malinzi hataki masihara
  "Baada ya hapo timu na mchezaji, watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Na kumbuka kanuni ya 68 (8) inataka kulipia kiasi cha sh 50,000 kwa kila mkataba wa mchezaji. Ni matarajio yetu kuwa kila klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu. Tunategemea kupata ushirikiano," imesema taarifa ya TFF.
  Kadhalika, kwa mujibu wa kanuni 67 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania ya StarTimes, TFF inakumbusha kwamba halitatoa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili.
  "Kila timu inatakiwa kuleta nakala tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na mchezaji mtakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Na kumbuka kanuni ya 67(8) inataka kulipia kiasi cha sh 25,000 kwa kila mkataba wa mchezaji,"imesema TFF.
  Taarifa ya TFF pia imesema katika hili inategemea kila timu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YACHIMBA MKWARA; "HUNA MKATABA, HUCHEZI LIGI KUU" Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top