• HABARI MPYA

  Wednesday, July 20, 2016

  TUZO ZA LIGI KUU BADO ZINA MUSHKELI

  JUMAPILI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi na wadhamini, walikabidhi tuzo za washindi mbalimbali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayorushwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam.
  Katika shughuli hiyo iliyofanyika hoteli ya Double Tree By Hilton, Masaki, Dar es Salaam, beki wa Yanga, Juma Abdul Jaffar Mnyamani alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu dhidi ya beki mwenzake, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba na kiungo wa Mtibwa Sugar, Shizza Kichuya.
  Na kwa ushindi huo, Abdul mbali na kukabidhiwa taji na mgeni rasmi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, pia atazawadiwa fedha Sh Milioni 9.2 wakati klabu yake, Yanga SC itazawadiwa Sh. Milioni 81.3 kwa kuwa bingwa, huku Sh. Milioni 40.6 zikienda kwa washindi wa pili, Azam FC, Sh Milioni 29 zikienda kwa washindi wa tatu, Simba SC na Sh. Milioni 23.2 zikienda kwa Prisons washindi wa nne.
  Aishi Salum Manula wa Azam FC alishinda tuzo ya kipa Bora akiwaangusha Deo Munishi ‘Dida’ wa Yanga na Benno Kakolanya wa Prisons na kuzawadiwa Sh. Milioni 5.7 huku mfungaji bora Amissi Tambwe wa Yanga akizawadiwa pia Sh. Milioni 5.7.
  Thabani Michael Kamusoko alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni, akiwaangusha Mzimbabwe mwenzake anayecheza naye Yanga SC, Donald Ngoma na kipa Muivory Coast wa Simba, Vincent Agban hivyo kuzawadiwa Sh. Milioni 5.7 pia.
  Mholanzi Hans van der Pluijm alishinda tuzo ya Kocha Bora na kuzawadiwa Sh. Milioni 8, akiwaangusha Mecky Maxime wa Mtibwa Sugar na Salum Mayanga wa Prisons.
  Tshabalala alishinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi akiwaangusha Farid Mussa wa Azam na Shizza Kichuya wa Mtibwa Sugar na kuzawadiwa Sh. Milioni 4.
  Ibrahim Hajib wa Simba alishinda tuzo ya Bao Bora la Msimu na kuzawadiwa Sh. Milioni 3 akimuangusha Tambwe wa Yanga, wakati Mtibwa Sugar imezibwaga JKT Ruvu na Mgambo Shooting katika tuzo ya Timu yenye Nidhamu na kuzawadiwa Sh. Milioni 17.2.
  Ngole Mwangole alishinda tuzo ya Refa Bora na kuzawadiwa Sh. Milioni 5.7 baada ya kuwaangusha Anthony Kayombo na Rajab Mrope.
  Nichukue fursa hii kuwapongeza TFF, Bodi ya Ligi na wadhamini wao kwa kufanikisha zoezi hilo- lakini pia kuelezea mapungufu niliyoyabaini ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuboresha tuzo hizo.
  Nilianza kuwa na maswali kuhusu tuzo mapema tu baada ya kutoka kwa orodha fupifupi za mwisho za waliongia fainali ya kuwania tuzo.
  Nilistaajabishwa na kukosekana kwa baadhi ya wachezaji kama kipa wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’, beki wa Azam FC, Shomary Kapombe na mshambuliaji wa Stand United Elias Maguri.
  Lakini sikutaka kuchukua hatua mapema, kwa kusubiri sifa na vigezo vya waliochukuliwa vitajwe labda kuna yale nisiyoyajua. 
  Lakini mwisho wa siku, nikabaini tu ni Kamati ya Tuzo, ilijiridhisha iliyowachukua ni bora kuliko iliyowaacha.
  Ally Barthez ni kipa aliyedaka sehemu kubwa ya msimu katika Ligi Kuu Yanga SC, kabla ya kuumia mwishoni kabisa na Deo Munishi ‘Dida’ akamalizia msimu vizuri.
  Shomary Kapombe alikuwa mchezaji nyota wa Azam FC karibu katika kila mechi na mwisho wa msimu akawa beki aliyefunga mabao mengi zaidi (saba) katika Ligi Kuu.
  Elias Maguri ni mshambuliaji mzawa aliyefunga mabao mengi zaidi, 14 na kushika nafasi ya nne katika chati ya wafungaji wa Ligi Kuu, nyuma ya Tambwe Amissi wa Yanga mabao 21, Hamisi Kiiza wa Simba SC, mabao 19 na Donald Ngoma 17.
  Pamoja na yote, wachezaji hawa hawakuishawishi Kamati ya Tuzo kuwaingiza fainali. 
  Dosari nyingine inayojitokeza ni kwenye tuzo ya jumla ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu kugeuzwa kama Tuzo ya Mchezaji Bora Mzawa wa Ligi Kuu na kwa sababu hiyo kukawa na Tuzo Mchezaji Bora wa Kigeni.
  Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi inapaswa kwenda kwa mchezaji aliyefanya vizuri zaidi katika msimu husika bila kujali kama ni mzawa au mgeni na kwa sababu hiyo hatutaona tena umuhimu wa kuwa na Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kigeni.
  Na hivyo ndivyo ilivyo hata kwa Ligi Kuu za wenzetu zilizopiga hatua kubwa, mfano England mwaka huu Jamie Vardy amekuwa mzawa wa kwanza kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu baada ya wageni mfululizo, Nemanja Vidic (Serbia), Vincent Kompany (Ubelgiji), Gareth Bale (Wales), Luis Suarez (Uruguay) na Eden Hazard (Ubelgiji), tangu Wayne Rooney alipotwaa mara ya mwisho mwaka 2010.
  Farid Mussa wa Azam aliingia katika kipengele cha Mchezaji Bora Chipukizi, lakini akashindwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
  Sipingani na walioamua hivyo, lakini kila naporudia kazi za wawili hao msimu uliopita sioni Tshabalala anaupata wapi ubora wa kumzidi Farid.
  Farid alikuwa ana msimu mzuri zaidi, baada ya kuisaidia Azam kutwaa Kombe la Afrika Mashariki na Kati akaingia na moto wake katika Ligi Kuu hadi kufanikiwa kucheza mechi yake ya kwanza kimataifa dhidi ya Nigeria.
  Na akaendelea kuichezea Taifa Stars kama mchezaji tegemeo tangu hapo na mwishoni mwa msimu akaenda kwenye majaribio Hispania ambako iliripotiwa amefuzu.
  Farid aliiweka Azam katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu na Tshabalala ambaye bado hajapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Taifa Stars, akaiweka Simba nafasi ya tatu. Nani bora hapa? 
  Nikiri kuna mabadiliko makubwa katika tuzo za Ligi Kuu mwaka huu kutoka miaka miwili iliyopita, ambayo tulishuhudia ‘mazingaombwe’ ya kutisha.
  Lakini bado kuna mapungufu kidogo, ambayo TFF na Bodi ya Ligi wanapaswa kuyafanyia kazi ili kuondoa ukakasi ambao umekuwa ukijirudia sasa bila sababu za msingi.
  Unawezaje kumuacha Kapombe, Dida na Maguri katika orodha ya wawania tuzo baada ya kurejea kazi waliyoifanya msimu uliopita? Tuzo za Ligi Kuu bado zina mushkeli.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TUZO ZA LIGI KUU BADO ZINA MUSHKELI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top