• HABARI MPYA

    Friday, July 15, 2016

    TFF YATAKA AIRTEL RISING STARS IPEWE UMUHIMU NA MIKOA YOTE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limewataka viongozi wa soka wa mikoa nchini kuyapa umuhimu mashindano ya vijana chini wa umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars ambayo lengo lake kuu ni kuibua vipaji vya soka.
    "Inaonekana kwamba baadhi ya viongozi wa mikoa wamekuwa wamejikita zaidi katika kupata ushindi uwanjani bila kuweka mkazo wa kutafuta vipaji vipya vinavyoibukia jambo ambalo limekuwa likichangia kudanganya umri kwa baadhi ya wachezaji kwenye programu za soka kama Airtel Rising Stars", alisema Katibu Mkuu TFF Celestine Mwesigwa.
    Mwesingwa alitoa pongezi za dhati kwa Airtel Tanzania kwa kuendelea kuwekeza kwenye soka la vijana Tanzania. ‘Airtel Rising Stars imekuwa ni nguzo muhimu kwenye maendeleo ya mpira wa miguu nchini na zaidi kwenye timu ya Taifa ya wanawake – Twiga Stars ambayo wachezaji wake wote wametokana na michuano ya Airtel Rising Stars, alisema Mwesigwa. 
    Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa (kushoto) akiongea na viongozi wa soka wa mikoa wakati ya semina elekezi ya Airtel Rising Stars iliyofanyika jijini Dar es Salaam Ijumaa, Julai 15 2016

    Huu ni mwaka wa sita kwa Airtel Tanzania kudhamini michuano hii ambayo inalenga kutafuta na kukuza vipaji vya soka nchini. Alisema miradi ya kukuza soka la vijana ndio njia pekee ya kukuza soka sehemu yeyote duniani. ‘Ghana, kwa mfano, imeweza kuendelea kufanya vizuri kwenye soka Afrika kwa kuwekeza kwenye soka la vijana – alisema Mwesigwa.
    Mwesigwa alitoa wito kwa viongozi wa soka kufuatilia na kutii sheria na kanuni ambazo zinaongoza michuano ya Airtel Rising Stars. ‘Naomba muelewe ya kwamba hii michuano ni muhimu zaidi kwa sababu mnafanya kazi na vijana ambao wanatikiwa kuongozwa kwa umakini wa hali ya juu sana’, alisema Mwesigwa. ‘Ukimfundisha kumheshimu mwamuzi atafanya hivyo kwa maisha yake yote ya soka lakini ukimfundisha kumdharau mwamuzi, pia atafanya hivyo katika maisha yake yote ya soka’, aliongeza Mwesigwa.
    Michuano ya Airtel Rising Stars inatarajiwa kuanza mwishoni mwezi huu katika ngazi ya mkoa na kufikia ukingoni Agosti 28 huku fainali za Taifa zikichezwa Dar es Salaam Septemba 6 mpaka 11 2016.
    Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano Airtel Tanzania Jane Matinde alisema michuano ya Airtel Rising Stars 2016 ni fursa nyingine kwa vijana kuonyesha vipaji vyao vya soka na kupata nafasi ya kutimiza ndoto zao. 
    Matinde aliongeza kuwa Airtel Rising Stars 2016 imeungana na promosheni ya Airtel Tanzania maarufu kama ‘Airtel Fursa’ ambayo inalenga kusaidia vijana wenye miradi yao ya maendeleo ambayo imeshindwa kupata Mafanikio kwa kukosa mitaji.
    Michuano hiyo kwa mwaka itashirikisha mikoa ya Mwanza, Morogoro, Mbeya, Temeke, Ilala na Morogoro kwa wavulana na Ilala, Kinondoni, Temeke, Lindi, Zanzibar na Arusha kwa wanawake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YATAKA AIRTEL RISING STARS IPEWE UMUHIMU NA MIKOA YOTE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top