• HABARI MPYA

  Sunday, July 17, 2016

  SIKU MANJI AKIONDOKA, ATAIACHAJE YANGA?

  UKITAKA kuwaudhi wana Yanga, hoji chochote kuhusu mwenendo wa Mwenyekiti wao kipenzi, Yussuf Manji katika klabu hiyo.
  Watakutukana matusi yote, kwa sababu wao wanachopenda kusikia ni Mwenyekiti wao huyo akisifiwa tu, bila kuzingataia mustakabali wa klabu yao ukoje chini ya mfanyabiashara huyo.
  Hawataki kujiuliza itakuwaje Yanga yao siku Manjii akiondoka – wakati yeye mwenyewe amekwishasema siku moja ataondoka.
  “Yanga ilikuwepo kabla yangu na itakuwapo baada yangu.  Ni wajibu wangu kuiacha Yanga ikiwa klabu bora zaidi kuliko nilivyoikuta na nikiona siwezi tena kutumikia maslahi ya wanachama wake, sitasita kujiuzulu au kuitisha uchaguzi ili kujipanga upya,”.
  Manji alisema maneno hayo hivi karibuni wakati akitolea ufafanuzi taarifa mbalimbali likiwemo suala la kusitisha Mkataba wa udhamini na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).  
  Manji alisema kwamba alilazimika kuuvunja Mkataba wa TBL kutokana na kwamba ulikuwa haramu na ameingia Mkataba na Kampuni ya International Marketing ili iitafutie klabu wafadhili wengine wa kuziba pengo la TBL. 
  "Mkataba wa kampuni ya bia nchini (TBL) na Yanga ulisainiwa miaka mitano iliyopita na mtangulizi wangu.  Huu ulikuwa mkataba haramu, kwani mamlaka ya kutia saini mikataba kwa mujibu wa Katiba ya Yanga yapo kwa wadhamini na hapana kitu kama azimio kutoka  bodi ya wadhamini kuingia katika makubaliano kama haya, au mkataba kusainiwa na wadhamini,”alisema.
  Manji alisema katika kipindi chake kilichopita alijitahidi kurekebisha tofauti zote zilizokuwepo kwenye Mkataba huo, lakini alishindwa. 
  Yanga waliachana na TBL rasmi mwezi uliopita kwa kuvaa jezi za Quality Group na Manji akaishutumu TBL ni mara moja tu imetoa Sh. 20 Millioni kwa ajili ya tamasha la Yanga Day zilizoahidiwa kutolewa kila mwaka.
  Akadai pia TBL haijailipa klabu fedha ya marekebisho inayofikia Sh. 30 Milioni wala haijawapa basi kwa kiwango sahihi tulichotaka kama ililoahidi katika mkataba na kwamba waliijulisha, lakini haijalishughulikia.
  Manji akasema International Marketing ni kampuni ambayo alikuwa Mwenyekiti wake na ikakubali ufadhili huo wa mwezi mmoja, jambo ambalo liliifanya Yanga kuvaa jezi za nembo yake Quality Group katika mchezo dhidi ya TP Mazambe.
  "Iwapo wanachama wa Yanga wakihisi nilivunja katiba kwa maslahi yangu binafsi au wakiwa na sehemu nyingine bora zaidi ya kufanya hivyo, walifikishe suala hilo kwenye Kamati ya Maadili ya klabu kwa ajili ya uamuzi.
  Manji aakaongeza kwamba achaguliwa katika mazingira ya amani zaidi miongoni mwa vyama vya soka nchini na ambapo hakuna hata senti moja ilitumika kwa ajili ya kumhonga yeyote.
  Ndoa ya Yanga na TBL iliyodumu tangu mwaka 2008 inavunjika Juni 2016 kwa sababu ambazo sisiti kusema ni za kulazimishwa tu na Manji.
  TBL imekuwa ikitekeleza mambo yote ya msingi katika Mkataba wake na Yanga na ambayo hayakufanyika, basi utagundua chanzo ni klabu yenyewe.
  Lini klabu ilifanya tamasha la Yanga Day, TBL ikashindwa kutoa fungu? Mbona mahasimu wao, Simba ambao pia wapo chini ya TBL kila mwaka wanafanya tamasha la Simba Day na hawajawahi kulalamika kunyimwa fedha?
  Ikumbukwe Manji tayari ameijengea kama uadui Yanga na kampuni ya Azam Media, ambao ni wadhamini wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara upande wa haki za matangazo ya TV.
  Azam TV pia ni wadhamini wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Yanga iligomea udhamini wa Azam TV katika Ligi Kuu na imeendelea kuipinga Azam TV hata inapopewa kibali na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kurusha mechi za Kombe la Shirikisho.
  Ukiuliza haswa sababu za Manji kuwachukia Azam TV zaidi ya kile anachosema inakosea kutoa fedha kwa Yanga na Simba kama timu kubwa na sawa na timu nyingine ambazo hazina mashabiki wengi.
  Lakini siku zote mambo humalizwa mezani, je jitihada gani klabu ilifanya kuketi mezani na Azam TV kufikiria namna ya kulitatua hilo?
  Na Azam TV ina nia nzuri tu ndiyo maana ikaziongezea Simba na Yanga kipengele cha Simba TV na Yanga TV, vipindi maalum vya talevisheni vya klabu hizo ambavyo vingewafanya wapate fungu lingine zaidi. 
  Simba walisaini Mkataba wa Simba na TV na kila mwaka wanavuna cha juu kutoka mgawo wa kawaida wa haki za matangazo ya TV.
  Bado katika Mkataba mpya, Azam TV wamebadilisha vipengele na sasa timu zinazokamata nafasi za juu katika Ligi Kuu zitapata fedha zaidi ya zile za chini kuelekea mkiani.
  Manji aliingia Yanga akiwa tayari ana ugomvi na mfanyabiashara mwenzake na mwana Yanga wa siku nyingi, Reginald Mengi.
  Na akaanza kuitumia Yanga kama kinga katika ugomvi wake na Mengi akifikia hadi kuwatumia wazee na wanachama wa klabu hiyo ‘wasiojielewa’ kumshambulia Mengi ambaye ana historia ya mchango wa mali na mawazo ndani ya klabu.
  Manji amepiga hatua zaidi na sasa anaijengea uadui Yanga na TFF licha ya kile kilichoonekana wazi wazi, msimu uliopita klabu hiyo ‘ilibebwa’ na shirikisho hilo hadi kufanikiwa kutwaa mataji yote matatu ya nyumbani, Ngao ya Jamii, Kombe la TFF na Ligi Kuu.
  Hakuna haja ya kupindisha maneno hapa, taswira nzima ya TFF ni Yanga tupu, Rais Jamal Malinzi, Katibu Selestine Mwesigwa hadi watendaji wengine kibao wa kuajiriwa na Wajumbe wengi wa Kamati mbalimbali ni Yanga wa kutupwa.
  Na hao ndio wapo nyuma ya mafanikio ya Yanga msimu uliopita – lakini pamoja na ukweli huo, bado Manji anagombana na TFF.
  Katika kipindi kifupi tu cha Manji kuwa Mwenyekiti wa Yanga imegombana na TBL, Mengi, Azam TV na TFF na sijui baada ya miaka minne ijayo akimaliza muda wake wa kuwa madarakani idadi itakuwa imeongezeja kiasi gani.
  Na wakati huo huo, tayari amekwishawaambia wana Yanga, kwamba yeye klabu aliikuta na ataiacha siku yoyote mambo yakimshinda.
  Na akiondoka ataondoka na ofa zake zote zikiwemo za kuipelekea timu kambini Uturuki, kusajili wachezaji wa kawaida kwa bei kubwa, kuajiri makocha wa kigeni.
  Wachezaji kulala hoteli za hadhi za juu, na gharama zote anazotumia sasa kuendesha klabu, ikiwemo fedha za kulipia viwanja vya kukodi kwa ajili ya mazoezi kila siku, vyote vitakoma. Ataiachia klabu mzigo mkubwa wa uendeshaji kulingana na mfumo uliopo sasa wa malipo makubwa ya mishahara na matumizi ya gharama kubwa bila sababu.
  Na mbaya zaidi ataondoka akiichia klabu ugomvi na watu na taasisi kibao – maana yake viongozi watakaomfuatia sasa waanze tena kubembeleza kuirudishia mahusiano mazuri klabu.
  Yanga wanashindwa kuelewa kwamba Manji anaifanya klabu yao kila siku izidi kukonda kiuchumi huku yeye akiwa tegemeo la kila kitu kuhusu klabu.
  Na katika utawala wake, yapi anafanya kwa faida ya klabu kwamba hata akiondoka atakumbukwa kwa kitu fulani aliifanyia Yanga?
  Kambi za nje ya nchi Yanga zilifanyika tangu wakati wa marehemu Tarbu Mangara timu ilikwenda hadi Brazil – hivyo hayo ya kwenda Uturuki yatakuwa sehemu ya historia tu, Manji atakumbukwa kwa lipi Jangwani?
  Jengo la makao makuu ya klabu linaoza, hali ya Uwanja wa Kaunda inazidi kuwa mbaya kila uchao na amekuwa mtu mjanja anayejua kucheza vizuri na akili za wana Yanga.
  Wakati mwingine anawatumia wana Yanga hao hao kuhalalisha sababu za kutoitimizia klabu ahadi za muhimu kama ujenzi wa Uwanja au ukarabati wa jengo.
  Makao makuu ya Yanga ni kitegauchumi kikubwa ambacho kimeachwa tu hakina faida yoyote na wanachama wa klabu hiyo wanafurahia usajili wa Thabani Kamusoko na Ngoma wakati klabu yao inazidi kuathirika kiuchumi kila kukicha.
  Yanga sasa wamekwishazoea kufanyiwa kila kitu na Manji na wamesahau kabisa mpango wa kuifanya klabu yao ijimudu yenyewe.
  Na mbaya zaidi, Manji anaijengea klabu uadui na watu na tasisi muhimu kila kukicha.
  Na hapo ndipo ninapojiuliza, siku Manji akiondoka ataiachaje Yanga? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIKU MANJI AKIONDOKA, ATAIACHAJE YANGA? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top