• HABARI MPYA

    Friday, June 17, 2016

    YANGA WAWASILI SALAMA BEJAIA, WAFIKIA RAYA HOTEL

    Na Mwandishi Wetu, BEJAIA
    YANGA SC imewasili salama mjini Bejaia, Algeria mchana wa leo, tayari kwa mchezo fungua dimba wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika Jumapili dhidi ya wenyeji, Mouloudia Olympique Bejaia.
    Yanga imefikia katika hoteli ya kifahari ya Raya mjini humo na leo baadaye itafanya mazoezi Uwanja wa jirani, kabla ya kesho kufanya mazoezi Uwanja wa Unite Maghrebine ambao utatumika kwa mchezo wa Jumapili.
    Yanga imewasili kutoka mjini Antalya, Uturuki ambako iliweka kambi katika hoteli ya Rui tangu Jumapili.
    Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Morocco, Bouchaib El Ahrach atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera, Redouane Achik na Youssef Mabrouk.
    Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma anatarajiwa kuiongoza timu yake dhidi ya MO Bejaia Jumapili
    Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kuwakaribisha mabingwa wa Afrika, TP Mazembe Juni 28 katika mchezo wake wa pili wa Kundi A.
    Na katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechanganya marefa kutoka nchi tatu tofauti, ambao ni Janny Sikazwe wa Zambia atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Jerson Emiliano Dos Santos wa Angola na Berhe O'michael wa Eritrea.
    Timu nyingine katika Kundi A ni Medeama ya Ghana ambayo itafungua dimba na TP Mazembe mjini Lubumbashi Juni 17, mwaka huu, mchezo ambao utachezeshwa na marefa wa Shelisheli Bernard Camille, Hensley Danny Petrousse na Eldrick Adelaide.
    Kikosi kamili cha Yanga kilichopo kambini Uturuki ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.
    Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
    Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na Godfrey Mwashiuya.
    Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.
    Msafara upo chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAWASILI SALAMA BEJAIA, WAFIKIA RAYA HOTEL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top