• HABARI MPYA

  Sunday, June 19, 2016

  YANGA ISICHEZEE SHILINGI CHOONI, SUALA LA KESSY SAWA NA BOKUNGU

  UWEZEKANO wa beki Hassan Ramadhan ‘Kessy’ kuanza kuichezea Yanga leo ni mdogo.
  Hiyo inafuatia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuomba barua ya Kessy kuruhusiwa na klabu yake ya zamani, Simba SC kuhamia Yanga.
  Inadaiwa rasmi Mkataba wa Kessy unamalizika mwezi huu na ili aanze kuichezea Yanga anatakiwa kuwa na barua ya kuruhusiwa kuondoka na Simba.
  Habari ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imezipata jioni ya jana zilisema kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliwatafuta viongozi wa Simba kuwaomba waandike barua ya kumruhusu Kessy kuondoka.

  “TFF wanatuomba tuwe waungwana tuandike hiyo barua ili huyo kijana acheze kesho, sasa bahati mbaya wanatuambia Jumamosi jioni na kila mtu amepumzika nyumbani kwake, ofisi zimefungwa,”alisema kiongozi mmoja wa Simba, ambaye hakutaka kutajwa jina.
  “Wavute subira, Jumatatu siyo mbali, tutalifanyia kazi hilo suala, ila kwa leo au kesho kulifanyia kazi hilo suala ni vigumu,” aliongeza.
  Yanga leo usiku itamenyana na Mouloudia Olympique Bejaia Uwanja wa Unite Maghrebine katika mchezo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika mjini Bejaia.
  Na kocha Pluijm alimtegemea Kessy kuziba pengo la majeruhi Juma Abdul, ambaye amebaki Dar es Salaam na sasa atakuwa hana namna nyingine zaidi ya kumpanga Mbuyu Twite beki ya kulia.
  Na ikumbukwe Kessy hakuondoka vizuri Simba, kwani baada ya kutoa pasi fyongo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Yanga Februari 2, mwaka huu na Donald Ngoma akaifungia Yanga katika ushindi wa 2-0, alianza kushukiwa kuhujumu timu.
  Na kitendo cha kusaini Yanga kabla ya msimu kumalizika kabisa kiliwaudhi Simba na kuamini walikuwa wanaishi na 'mamluki', hivyo inatarajiwa kabisa Wekundu wa Msimbazi hawatatoa ushirikiano katika hili.
  Hii maana yake Yanga wanapaswa kuwa makini mno na maamuzi yoyote yatakayohusu kumtumia Kessy leo, au mchezaji mwingine yeyote mpya aliyeingia katika usajili huu mdogo wa CAF.
  Wasidanganywe eti kwa kuwa CAF imetoa leseni kwa Kessy kucheza basi wamtumie. Si kweli. Si kweli kabisa.
  Kwani mwaka 2011, TP Mazembe iliwahi kupatwa na matatizo kwa kumtumia mchezaji ambaye CAF iliwapa leseni acheze.
  Na tunakumbuka vizuri matatizo ya Mazembe kwa sababu yalisababishwa na klabu ya hapa kwetu, Simba SC.
  Simba ilicheza Ligi ya Mabingwa mwaka huo ikianza kwa kuitoa Elan Mitsoudje ya Comoro kabla ya kwenda kukjutana na TP Mazembe.
  Simba ilitolewa kwa jumla ya mabao 6-3 ikifungwa 3-1 Lubumbashi na 3-2 Dar es Salaam.
  Lakini Simba ilirudishwa mashindanoni baada ya kushinda rufaa waliyomkatia beki wa Mazembe, Janvier Besala Bokungu, aliyevunja mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia.
  Simba ikacheza mechi ya mkondo mmoja na Wydad Casablanca ya Morocco mjini Cairo, Misri na kufungwa 3-0, hivyo kuangukia kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa mabao 2-1. 
  Hakuna Ofisa wa CAF anayeweza kuzungumza upuuzi eti leseni ndiyo kila kitu, huyo atakuwa mtu aliyechukuliwa na kuletwa kwenye soka, lakini bado hajafahamu vizuri.
  Janvier Besala Bokungu alikuwa ana leseni ya CAF, lakini mwisho wa siku CAF hao hao wakaiondoa mashindanoni Mazembe kwa sababu mchezaji alivunja Mkataba kinyume cha sheria.
  Mara nyingi usajili wetu huanza Juni na Simba wenyewe wanasema rasmi mwezi huu ndiyo Mkataba wa Kessy utamalizika – na kwa sababu hawawezi kutoa leseni ya mchezaji huyo, Yanga isichezee shilingi chooni.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA ISICHEZEE SHILINGI CHOONI, SUALA LA KESSY SAWA NA BOKUNGU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top