• HABARI MPYA

  Monday, June 06, 2016

  UKIMCHUKIA CHRISTIAN BELLA UNATAFUTA VIDONDA VYA TUMBO

  KUNA rafiki yangu mmoja mwandishi wa habari mnazi mkubwa wa Liverpool alikuwa akipata shida sana na Cristiano Ronaldo enzi hizo akiitumikia Manchester United.
  Alikuwa akikerwa  na mafanikio ya Manchester United, lakini alikerwa zaidi na Ronaldo ambaye ndiye alikuwa chachu ya mafanikio hayo ya Manchester United kipindi hicho. Nilikuwa nikimwambia sentesi moja tu – “Ukimchukia Ronaldo utapata vidonda vya tumbo”.
  Naam kumchukia mtu mwenye uwezo mkubwa kwenye fani yake ni kutafutia maudhi maradufu – Utachukia kila siku lakini chuki yako isisaidie lolote zaidi ya kukuletea vidonda vya tumbo kwa hasira za kujitakia.
  Niliwahi kusema hapo nyuma kuwa ipo tabia moja ambayo sijui dawa yake itapatikana lini – tabia ya kuwachukia wenye kujua, kuwaonea choyo, kuwaombea mabaya, yaani mtu anakonda  kwa mafanikio ya mwenzie, ananenepa kwa anguko la mwenzie.
  Nikabainisha kwamba kwenye sanaa tabia hii ndio imevuka mipaka, kuna chuki za kufa mtu na nikamtaja mwimbaji Christian Bella kama mmoja wa watu wanaokumbana na kadhia ya tabia hiyo ya kikorosho. 
  Nikasema Bella anaambiwa ana roho mbaya, anaringa lakini mbaya zaidi ni kwamba baadhi ya wasanii wa dansi na baadhi ya mashabiki wa muziki wa dansi wanatamani kumtenga Bella – eti hapigi dansi, anapiga bongo fleva - mada ya kijinga kabisa ambayo kama utaifuatilia kwa kina hutapata jibu la uhakika kuwa muziki wa dansi ni upi na bongo fleva ni ipi.
  Wasanii wa dansi wanaomchukia Bella naona wanajitafutia vidonda vya tumbo bure. Huyu mtu yuko ‘levo’ nyingine, si saizi yao tena na sasa watakaonufaika ni wale tu watakaomua kumuunga mkono, lakini watakaoendelea kumpinga watazimika kwenye ‘game’ kama mshumaa kwenye upepo. Huu ni ukweli usio na shaka.
  Bella wa leo sio wa jana. Tazama anavyokwea vidato kutoka hatua moja kwenda nyingine. Onyesho lake la Jumamosi usiku pale Escape One kwa kiingilio cha shilingi elfu 20 na 50, linajipambanua wazi kuwa jamaa anapanda ngazi kwa kasi ya ajabu.
  Huyu ni mwanamuziki aliyepotea kwenye kumbi za muziki kwa zaidi ya miezi minne akiwa mapumzikoni Sweden, lakini bado ameweza kurudi sokoni kwa kishindo tena bila hata ya kutegemea ‘mbeleko’ ya nyimbo mpya.
  Bella amemaliza kurekodi wimbo mpya “Nishike” lakini hakuahangaika kuuachia kuelekea onyesho lake hilo la Escape One na badala yake akajiamini kupitia kazi zake za nyuma. 
  Nilishasema kuwa anachokifanya Bella ni kusoma soko la muziki linahitaji nini kisha anapenya hapo hapo na iwapo wasanii wa dansi wataendelea kukaa kitako na kumtenga basi wataishia kusema jamaa hapigi dansi huku mwenzao akitengeneza pesa. Angalia namna makampuni makubwa yanavyoanza kumkimbilia Bella.
  Lakini pia Bella anajua ni namna gani staa anatakiwa kuishi, Bella si mtu utakayemuona ovyo ovyo mitaani au kwenye bar akicheza ‘pool table’. Bella anajua moja ya thamani ya msanii ni kuwa adimu machoni mwa watu ili wawe na kiu ya kukuona kazini au kupitia vyombo vya habari. Kipo cha kujifunza kwake badala ya kumchukia.
  Mtazame pia namna Bella alivojitengeneza na kuwa ‘jeshi la mtu mmoja’ ambaye anajitosheleza yeye mwenyewe bila kujali anafanya kazi na kundi la aina gani ya wasanii. Huu ndiyo mfumo unaotumiwa na wasanii wengi nyota duniani, mfumo unaokufanya usinyanyasike na msanii yeyote anayekutumikia, lakini pia ni mfumo unaomfanya tajiri anayekumiliki (kama yupo) awe na adabu.
  Sijui ni mara ya ngapi narudia hii kitu: Enzi za kufanya muziki kama wito zimepita, muziki wa sasa ni ajira, muziki ni maisha, ubunifu wa hali ya juu unahitajika na msanii anapaswa kubadilika kadri soko linavyobadilika.
  Bella ndiye mwanamuziki pekee wa dansi anayeweza kuwapiga vikumbo nyota wa bongo fleva kwenye soko la muziki, ifike wakati sasa wasanii, mashabiki na wadau wa dansi tumtumie Bella kama balozi wa mageuzi ya soko la dansi, tumuunge mkono ili njia zifunguke kwa wengine wengi. Kwanini upate vidonda vya tumbo kwa kumchukia mtu aliyekuzidi? Mi simo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: UKIMCHUKIA CHRISTIAN BELLA UNATAFUTA VIDONDA VYA TUMBO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top