• HABARI MPYA

    Sunday, June 05, 2016

    TFF WANACHEMKA, MANJI NAYE KWA NINI AUBURUZE UCHAGUZI WA YANGA?

    MVUTANO umeibuka kuhusu uchaguzi wa Yanga SC ambao sasa unawaacha njia panda wanachama wa klabu hiyo, wakiwa hawajui washike lipi.
    Hiyo inafuatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza na kuendesha mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo - wakati huo huo Yanga nayo ikitangaza na kuendesha mchakato wake huo yenyewe.
    Yanga imesema uchaguzi wake utafanyika Juni 11 na na TFF imesema utafanyika Juni 25. Na wote, TFF na Yanga wamenza kutoa fomu za kugombea wiki hii. 

    Waliochukua fomu TFF ni Aaron Nyanda, Titus Osoro wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Omari Said kutoka Zanzibar wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji, wakati miongoni mwa waliochukua fomu Yanga ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ayoub Nyenzi.
    Wakati mvutano huo, ukiendelea uongozi wa Yanga ukaibua tuhuma za TFF kwa kushirikiana na Kamati yake ya Uchaguzi chini ya Mwenyekiti, Wakili Alloyce Komba kupanga njama za kumkata Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji.
    Kwa tuhuma hizo, juzi Wakili Komba alitangaza kujitoa kusimamia mchakato wa uchaguzi wa Yanga.
    Inatuacha njia panda kidogo, Komba kutuhumiwa tu anajiuzulu – sasa tuelewe vipi kwamba amekimbia baada ya kutuhumiwa kwa ukweli, kupakaziwa au?
    Si gumu wala zito hilo la Komba, kubwa ambalo ninataka kuliwasilisha leo hapa ni juu ya huu mvutano wa uchaguzi wa Yanga kufanywa na vyombo viwili tofauti.
    Kwanza niseme, haya ni mambo ya fedheha na yamepitwa na wakati. Katika Tanzania ya leo kuturudisha enzi za migogoro isiyo na kichwa wala miguu ni kujiangusha wenyewe.
    Hakuna sababu ya TFF na Yanga kufikishana hapa, tunaamini kuna mapungufu katika mchakato mzima wa uchaguzi wa Yanga kwa sasa iwe ufanywe na TFF au klabu yenyewe na hivyo busara inahitajika ili wavuke katika kipindi hiki na kuingia zama mpya.
    Uongozi wa Yanga umepitisha muda wa kuwa madarakani, ni kweli – lakini bado hiyo haihalalishi uchaguzi wao kufanywa na TFF, labda vyombo hivyo viwili vishirikiane bega kwa bega katika zoezi hilo.
    Na uzuri utaratibu uko wazi, kwamba baada ya taratibu za awali Yanga watahamishia mchakato huo TFF kwa uhakiki – hivyo hakuna sababu ya kufika hapa watu wazima kulumbana kama watoto wadogo kwenye vyombo Habari.
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi asikubali tu kufanyia kazi maagizo hata yenye mapungufu kisa yametoka kunakoitwa kwa wakubwa.
    Dunia ya sasa ni ya uwazi wa ukweli na hata wakubwa wanakosea – Serikali haiwezi kuiambia TFF ifanye uchaguzi wa Yanga na makosa.
    Kweli Yanga wamekosea kwa kupitisha muda wa kuwa madarakani – lakini haiwezekani lifanyike kosa lingine leo kwa uchaguzi wa klabu hiyo kufanywa na TFF.
    Kinachotakiwa kwa sasa ni kusitisha zoezi lolote la uchaguzi wa Yanga kwa sasa na TFF ikutane na viongozi wanaotambulika wa klabu hiyo, wakae pamoja na kujadili namna nzuri ya kuendesha zoezi hilo.
    Na pia, uchaguzi wa Yanga hauwezi kufanyika ndani ya wiki mbili za kutangazwa kwake kama anavyotaka kufanya Manji. Haiwezekani. 
    Yanga ni taasisi kubwa, lazima upatikane muda wa kutosha kwa ajili ya uchaguzi, kuanzia kuutangaza na mazoezi mengine ya uchukuaji fomu, kurudisha, usaili, pingamizi na kadhalika.
    Leo Manji anakutana na Waandishi wa Habari Mei 30 kuwaambia uchaguzi wa Yanga utakuwa Juni 11, kweli? Kubwa kwangu leo, TFF na Yanga wakutane, waketi kukubaliana namna nzuri ya kulipitisha salama zoezi hili.    Kila la heri. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF WANACHEMKA, MANJI NAYE KWA NINI AUBURUZE UCHAGUZI WA YANGA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top