• HABARI MPYA

    Saturday, June 04, 2016

    TAIFA STARS LA KUVUNDA, SAMATTA AKOSA PENALTI…MISRI YAUA 2-0 TAIFA ZOTE SALAH

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MISRI imekata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Gabon, baada ya kuwafunga wenyeji, Tanzania mabao 2-0 jioni ya leo uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Matokeo hayo yanawafanya Misri wamalize mechi za Kundi G wakiwa na pointi 10 baada ya mechi nne, wakishinda tatu na kutoa sare moja, wakati Tanzania inabaki na pointi yake moja na inashika mkia nyuma ya Nigeria yenye pointi mbili.
    Hadi mapumziko, tayari Misri walikuwa mbele kwa 1-0 bao lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Chelsea ya England, Mohammed Salah dakika ya 43 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki Mwinyi Hajji Mngwali kumkwatua nje kidogo ya boksi Nagram Fahmy.
    Mohamed Salah akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza leo uwanja wa Taifa

    Katika kipindi hicho, timu zote zilishambuliana kwa zamu na kila upande ulipoteza nafasi za wazi.
    Dakika ya 27, mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu aliunganishia juu ya lango krosi ya Elias Maguri na dakika ya 30, Nahodha Mbwana Ally Samatta alipewa pasi nzuri na Farid Mussa akapiga nje.
    Kipindi cha pili, Taifa Stars walikianza vizuri na kufanikiwa kupata penalti dakika ya 53 iliyotolewa baada ya kiungo Himid Mao kuangushwa na Ame Medhat hata hivyo, mkwaju wa Nahodha Samatta ulipaa juu ya lango la kipa mkongwe barani, Essam Kamal Tawfik.
    Salah akaifungia bao la pili Misri dakika ya 58 baada ya kumpita beki wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali aliyecheza chini ya kiwango mno hii leo.
    Winga wa Tanzania, Farid Mussa (kulia) akimtoka kiungo wa Misri, Mohamed El Nenny 

    Kocha Charles Boniface Mkwasa akamtoa Mngwali baada ya kuchomesha kwa mara ya pili na kumuingiza Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, aliyekwenda kumalizia vizuri.
    Tanzania; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Mngwali/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk68, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Himid Mao, Thomas Ulimwengu/Deus Kaseke dk73, Mwinyi Kazimoto, Elias Maguli/John Bocco dk62, Mbwana Samatta na Farid Mussa.
    Misri; Essam Kamal Tawfik, Alg Gabr Mossad, Ramy Hisham Abdel, Mohamed Abdel Sayed, Abood Abdulrahamn Amed, Tarek Hamad Hamed, Mohamed Nasser Elsayed, Mohamem Ahmed Ibrahim/Amr Medhat dk63, Abdallah Mahamoud Said na Nagram Mohsin Fahmy.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS LA KUVUNDA, SAMATTA AKOSA PENALTI…MISRI YAUA 2-0 TAIFA ZOTE SALAH Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top