• HABARI MPYA

    Tuesday, June 21, 2016

    MAYANJA AREJEA 'KUPIGA NDIKI' MAANDALIZI YA MSIMU MPYA SIMBA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Simba, Mganda Jackson Mayanja anatarajiwa kuwasili Juni 25 au Juni 26 na siku moja baadaye ataanza programu ya mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya.
    Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe alipozungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo kuhusu mikakati ya usajili na maandalizi ya msimu mpya jana mjini Dar es Salaam.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Popppe amesema kwamba mara Mayanja atakapowasili, wachezaji wote wenye Mkataba na Simba SC wakiwemo wapya ambao wamesajiliwa hivi karibuni wataanza mazoezi.
    Kocha Jackson Mayanja anatarajiwa kuwasili Juni 25 au 26 kuanzisha mazoezini Simba SC 
    Poppe amesema kwamba kutakuwa na programu ya awali ya ‘amasha amsha’ mjini Dar es Salaam na mara baada ya kikosi kizima kukakamilika, timu itakwenda kuweka kambi rasmi ya kujiandaa na msimu mpya katika mkoa ambao utatajwa baadaye.
    Bado Poppe ameendelea kukataa majina ya wachezaji wapya waliosajiliwa Simba SC, ingawa BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE inafahamu hadi sasa waliosaini ni beki wa Mwadui FC, Emanuel Semwanza na viungo wa Mtibwa Sugar, Muzamil Yassin na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim.
    Kuhusu kocha mpya, Poppe amesema suala hilo bado linafanyiwa kazi na Kamati ya Ufundi, chini ya Mwenyekiti wake, Collin Frisch na mara litakapokamilika litawekwa wazi.
    “Mimi naomba niseme, sisi bado hatujajua kocha wetu na tupo kwenye mazungumzo na makocha watano, kati yao mmoja ndiye atakuwa kocha wa Simba, lakini kwa sasa bado hatujafikia mwafaka,”amesema Collin alipoulizwa na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo kuhusu mchakato huo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAYANJA AREJEA 'KUPIGA NDIKI' MAANDALIZI YA MSIMU MPYA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top