• HABARI MPYA

  Saturday, June 18, 2016

  CAF YAMPIGA STOP KESSY KUCHEZEA YANGA KESHO HADI AONYESHE BARUA YA SIMBA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  UWEZEKANO wa beki Hassan Ramadhan ‘Kessy’ kuanza kuichezea Yanga kesho ni mdogo.
  Hiyo inafuatia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuomba barua ya Kessy kuruhusiwa na klabu yake ya zamani, Simba SC kuhamia Yanga.
  Rasmi Mkataba wa Kessy unamalizika mwezi huu na ili aanze kuichezea Yanga anatakiwa kuwa na barua ya kuruhusiwa kuondoka na Simba.
  Habari ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imezipata jioni ya leo zinasema kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewatafuta viongozi wa Simba kuwaomba waandike barua ya kumruhusu Kessy kuondoka.
  Hassan Ramadhani 'Kessy' sasa anaweza kuukosa mchezo wa kesho wa Yanga dhidi ya MO Bejaia nchini Algeria

  “TFF wanatuomba tuwe waungwana tuandike hiyo barua ili huyo kijana acheze kesho, sasa bahati mbaya wanatuambia Jumamosi jioni na kila mtu amepumzika nyumbani kwake, ofisi zimefungwa,”amesema kiongozi mmoja wa Simba, ambaye hakutaka kutajwa jina.
  “Wavute subira, Jumatatu siyo mbali, tutalifanyia kazi hilo suala, ila kwa leo au kesho kulifanyia kazi hilo suala ni vigumu,” aliongeza.
  Yanga itamenyana na Mouloudia Olympique Bejaia Uwanja wa Unite Maghrebine katika mchezo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika mjini Bejaia kesho.
  Na kocha Pluijm alimtegemea Kessy kuziba pengo la majeruhi Juma Abdul, ambaye amebaki Dar es Salaam na sasa atakuwa hana namna nyingine zaidi ya kumpanga Mbuyu Twite beki ya kulia.
  Na ikumbukwe Kessy hakuondoka vizuri Simba, kwani baada ya kutoa pasi fyongo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Yanga Februari 2, mwaka huu na Donald Ngoma akaifungia Yanga katika ushindi wa 2-0, alianza kushukiwa kuhujumu timu.
  Na kitendo cha kusaini Yanga kabla ya msimu kumalizika kabisa kiliwaudhi Simba na kuamini walikuwa wanaishi na 'mamluki', hivyo inatarajiwa kabisa Wekundu wa Msimbazi hawatatoa ushirikiano katika hili. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CAF YAMPIGA STOP KESSY KUCHEZEA YANGA KESHO HADI AONYESHE BARUA YA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top