• HABARI MPYA

  Wednesday, May 18, 2016

  YONDAN AANZIA BENCHI YANGA NA SAGRADA ESPERANCA LEO

  Na Prince Akbar, GOA
  KOCHA wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amemuanzishia benchi beki Kevin Yondan katika mchezo dhidi ya Sagrada Esperanca mjini Dundo, Angola jioni ya leo.
  Pluijm amewaanzisha pamoja Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' na Mtogo, Vincent Bossou katika beki ya kati, wakati kulia anacheza Juma Abdul na kushoto Oscar Joshua wakimlinda kipa Deo Munishi 'Dida'.
  Pluijm amepanga viungo watatu, ambao wote ni wa kigeni, Mkongo Mbuyu Twite, Mnyarwanda Haruna Niyonzima na Mzimbabwe Thabani Kamusoko. Washambuliaji ni wageni pia, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma.
  Anayekamilisha orodha ya wachezaji 11 wanaoanza Yanga leo ni winga mzawa Simona Msuva, aliyefunga bao la kwanza katika ushindi wa 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam. 
  Kevin Yondan anaanzia benchi leo Yanga ikimenyana na Sagrada Esperanca nchini Angola

  Mchezo huo wa marudiano kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, unatarajiwa kuanza Saa 9:00 Alasiri kwa saa za Angola na Saa 11:00 jioni kwa Saa za Tanzania Uwanja wa Sagrada Esperanca.
  Yanga itahitaji sare ili kuingia hatua ya makundi, baada ya awali kushinda 2-0, mabao ya Msuva na Matheo Anthony wiki iliyopita Dar es Salaam.
  Mbali na Yondan, wengine wanaoanzia benchi leo ni Ally Mustafa 'Barthez', beki Mwinyi Hajji Mngwali, viungo Deus Kaseke, Geoffrey Mwashiuya na washambuliaji Matheo Anthony na Paul Nonga.
  Pluijm anaamini kurejea kwa wachezaji wake wawili Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donaldo Ngoma kutaiogezea nguvu timu yake. 
  Wawili hao waliukosa mchezo wa kwanza kutokana na kuwa wanatumikia adhabu ya kadi za njano walizopewa kwenye mechi mfululizo dhidi ya Al Ahly ya Misri mwezi uliopita Dar es Salaan na Cairo, Yanga ikitolewa kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya sare ya 1-1 nyumbani na kufungwa 2-0 ugenini.
  Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.
  Vikosi vya leo vinatarajiwa kuwa; Yanga; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Haruna Niyonzima.
  Sagrada Esperanca; Yuri Jose Tavazes, Roadro Juan da Semero, Dennis Conha Morais, Asenio Cabungula, Antonio da Silva Oliveira, Ntaku Zabakaka, Manuel Paulo Joao, Alentua Tangala Rolli, Osvaldochitumba Palana, Manuel Sallo Conha na Antonio Kasule. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YONDAN AANZIA BENCHI YANGA NA SAGRADA ESPERANCA LEO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top