• HABARI MPYA

  Sunday, May 08, 2016

  YANGA BINGWA LIGI KUU, MWADUI YAICHAPA SIMBA 1-0

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  YANGA SC ndiye bingwa mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/2016 ingawa wana mechi tatu za kumalizia dhidi ya Mbeya City, Ndanda FC na Majimaji, zote ugenini.
  Hiyo inafuatia Simba SC kufungwa bao 1-0 na Mwadui FC jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu.
  Matokeo hayo yanamaanisha hakuna timu yoyote ya Ligi Kuu yenye uwezo wa kufikisha pointi 68 ambazo wanazo Yanga hadi sasa – na bila ubishi timu ya Jangwani imetetea ubingwa.
  Simba SC ina pointi 58 baada ya kucheza mechi 27 na inaweza kufikisha pointi 67 ikishinda mechi zake zote tatu zilizobaki, wakati Azam FC inaweza kumaliza na pointi 66. 
  Bao lililoipa ubingwa Yanga leo lilifungwa dakika ya 73 na kiungo Jamal Simba Mnyate aliyemalizia pasi ya mshambuliaji Kevin Sabato baada ya mpira mrefu uliopigwa na kipa Jackson Abdulrahman.
  Mashabiki wa Yanga wakifurahia na Kombe bandia Uwanja wa Taifa

  Katika mchezo huo, Mwadui FC walipata pigo dakika ya 20 kufuatia kipa wake wa kwanza, Shaaban Hassan Kado kuumia baada ya kugongana na mshambuliaji wa Simba SC, Mganda Hamisi Kiiza wakati anakwenda kuokoa krosi ya Mrundi Emery Nimubona.
  Kipa wa akiba, Jackson Abdulrahman akachukua nafasi na kumalizia vizuri mchezo huo akichangia kupatikana kwa bao pekee la ushindi.
  Mshambuliaji wa Simba SC, Ibrahim Hajib alitolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya mwisho kati ya tatu za nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida za mchezo, kwa kumchezea rafu Hassan Kabunda.
  Mfungaji wa bao pekee la Mwadui, Jamal Mnyate akimtoka beki wa Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala' leo Uwanja wa Taifa
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Azam FC imeichapa mabao 2-1 Kagera Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Mabao ya Azam FC yamefungwa na Kipre Herman Tchetche na Himid Mao, wakati la Kagera limefungwa na Adam Kingwande. 
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Juuko Murshid, Justice Majabvi, Peter Mwalyanzi/Brian Majwega dk46, Said Ndemla, Hamisi Kiiza/Mussa Mgosi dk84, Hajji Ugando/Ibrahim Hajib dk46 na Mwinyi Kazimoto.
  Mwadui FC; Shaaban Kado/Jackson Abdulrahman dk20, Malika Ndeule, David Luhende, Iddy Mobby, Abdallah Mfuko, Jabir Aziz, Hassan Kabunda, Razack Khalfan, Kelvin Sabato/Salim Hamisi dk89, Rashid Mandawa/Julius Mrope dk69 na Jamal Mnyate.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA BINGWA LIGI KUU, MWADUI YAICHAPA SIMBA 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top