• HABARI MPYA

    Friday, May 13, 2016

    WASPANYOLA WATUA KUMRITHI STEWART HALL AZAM FC

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MAKOCHA wawili kutoka klabu ya Deportivo Tenerife ya Hispania wamewasili jioni ya leo kwa ajili ya kuja kufanya mazungumzo ya kusaini Mkataba wa kufundisha Azam FC.
    Makocha hao Jonas Garcia Luis na Zebensul Hernandez Rodriguez wamewasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam Saa 10:00 jioni kwa ndege ya Emirates na kupokewa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba.
    Mara baada ya kuwasili JNIA, makocha hao walisema kwamba wanatarajia kupata mwongozo wote kutoka wenyeji wao na wasingeweza kuzungumza mambo mengi.
    Kawemba alisema kwamba wawili hao wamekuja kwa mazungumzo ambayo kama yatakwenda vizuri wataajiriwa kwa ajili ya kufundisha timu kuanzia msimu ujao.
    Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba (kulia) akiwa na mmoja wa makocha waliowasili leo kutoka Hispania,  Zebensul Hernandez Rodriguez 
    Kawemba akiongozana na Rodriguez baada ya kuwasili JNIA jioni ya leo
    Saad Kawemba akiwa na Rodriguez (kulia) na  Jonas Garcia Luis (kushoto) 
    Wakala wa makocha hao, Royco Garcia akizungumza na Waandishi wa Habari nje ya JNIA

    Jonas Garcia Luis na Zebensul Hernandez Rodriguez (kulia) wakiwa ndani ya gari tayari kuondoka JNIA

    Kawemba amesema kwamba makocha hao watasafiri kwenda Tanga kesho kuiona timu ikicheza na African Sports katika mchezo wa Ligi Kuu kesho Uwanja wa Mkwakwani.
    Tayari kocha Muingereza, Stewart John Hall amekwishaaga kwamba ataondoka mwishoni mwa msimu, ambao unakamilika Juni.
    Habari ziadi ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inazo ni kwamba wawili hawa wametangulia na kuna makocha zaidi wanatarajiwa kuwasili kuunda benchi la zito la ufundi la Azam FC.  
    Kupatikana kwa makocha hao ni matunda ya winga chipukizi wa Azam FC, Farid Mussa kwenda kwenye majaribio Hispania.
    Farid amefuzu majaribio katika klabu ya Tenerife ya Daraja la Kwanza Hispania, na sasa klabu hiyo imeanza majadiliano na Azam FC juu ya biashara ya mchezaji huyo.
    Nyuma ya biashara hiyo, Azam na Tenerife wanaelekea kufunga ndoa nzito ambayo matunda yake ni ujio wa makocha hawa watakaofundisha kuanzia timu za vijana.
    Makocha hawa wanataka pia kubadilisha kabisa mfumo wa akademi ya Azam FC kwa kuchukua vijana wadogo zaidi kuanzia umri wa chini ya miaka 12.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WASPANYOLA WATUA KUMRITHI STEWART HALL AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top