• HABARI MPYA

  Sunday, May 08, 2016

  ULIMWENGU AUMIA MAZEMBE IKIPATA USHINDI MWEMBAMBA NYUMBANI

  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu (pichani kulia) amecheza kwa dakika 45 tu za kwanza timu yake, TP Mazembe ikishinda 1-0 katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika dhidi ya  Stade Gabesien ya Tunisia jioni ya leo Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi.
  Ulimwengu alitoka uwanjani anachechemea baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza na kipindi cha pili, Solomon Asante akachukua nafasi yake.
  Jonathan Bolingi akaifungia bao pekee Mazembe dakika ya 90 na ushei na sasa timu hiyo ya DRC ina kibaruwa cha kwenda kuulinda ushindi huo mwembamba Tunisia wiki ijayo.
  Katika mechi za jana, El Merreikh ya Sudan pia ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Kawkab Marrakech ya Morocco, nayo itatakiwa kwenda kuulinda ushindi huo kiduchu wiki ijayo mjini Marakech, Morocco. 
  Mechi nyingine za jana, Mouloudia Olympique de Bejaia ya Algeria ililazimishwa sare ya bila kufungana na Esperance ya Tunisia sawa na Stade Malien wa Mali waliolazimishwa sare ya 0-0 na FUS Rabat ya Morocco mjini Bamako.
  Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imeialza 3-1 Medeama ya Ghana Uwanja wa Lucas Moripe, Yanga SC ya Tanzania ikishinda 2-0 dhidi ya Sagrada Esperanca.
  Juzi zilichezwa mechi mbili, Ahli Tripoli ya Libya ililazimishwa sare ya 0-0 na Misr Makkassa na Etoile du Sahel wakishinda 2-0 dhidi ya C.F. Mounana.
  Mechi za kwanza za mchujo wa kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho zinahitimishwa leo kwa mchezo kati ya wenyeji, TP Mazembe na Stade Gabesien ya Tunisia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ULIMWENGU AUMIA MAZEMBE IKIPATA USHINDI MWEMBAMBA NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top