• HABARI MPYA

    Tuesday, May 17, 2016

    SMG AWAPA ‘TAFU’ LA MAANA YANGA ANGOLA

    Na Prince Akbar, DUNDO
    NYOTA wa zamani wa Yanga SC, Said Maulid ‘SMG’ ndiye mwenyeji wa timu yake hiyo ya zamani nchini Angola 
    Yanga ipo mjini Dundo, Angola kwa ajili ya mchezo wao wa kesho dhidi ya wenyeji, Sagrada Esperanca kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Na SMG ambaye alimalizia soka yake Angola kabla ya kuwa kocha, amewapokea Watanzania wenzake na timu yake ya zamani na kuisaidia kuelekea mchezo wa kesho.
    SMG anayeongea vizuri Kireno, lugha inayotumika Angola ndiye aliyeandaa kila kitu kwa ajii ya Yanga nchini Angola.
    SMG alijiunga na Yanga SC mwaka 2000, akitoka Simba SC aliyoichezea kwa mwaka mmoja tu na alidumu Jangwani hadi mwaka 2008 alipohamia Angola Onze Bravos do Maquis ambako alistaafu na kuwa kocha.
    Said Maulid 'SMG' (kushoto) akiwa na Godson Karigo, mmoja wa viongozi wa Yanga leo Uwanja wa Sagrada Esperanca mjini Dundo wakati wa mazoezi ya timu hiyo

    Yanga waliowasili jana usiku mjini Dundo baada ya kuondoka Dar es Salaam asubuhi wakipitia Luanda, wamefikia katika hoteli ya bora zaidi mjini humo, Diamante na leo jioni wamefanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sagrada Esperanca mjini hapa.
    Katika mchezo wa kesho, Yanga itahitaji sare ili kuingia hatua ya makundi, baada ya awali kushinda 2-0, mabao ya Simon Msuva na Matheo Anthony wiki iliyopita Dar es Salaam.
    Kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema kwamba ana imani kurejea kwa wachezaji wake wawili Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donaldo Ngoma kutaiogezea nguvu timu yake. 
    Wawili hao waliukosa mchezo wa kwanza kutokana na kuwa wanatumikia adhabu ya kadi za njano walizopewa kwenye mechi mfululizo dhidi ya Al Ahly ya Misri mwezi uliopita Dar es Salaan na Cairo, Yanga ikitolewa kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya sare ya 1-1 nyumbani na kufungwa 2-0 ugenini.
    Mechi ya kesho itachezeshwa na marefa wa Madagascar, Hamada el Moussa Nampiandraza atakayepuliza filimbi, akisaidiwa na washika vibendera Velomanana Ferdinand Jinoro na Jean Thierry Djaonirina.
    Wachezaji wa Yanga wakiomba dua kabla ya mazoezi yao mjini Dundo leo

    Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.
    Yanga ilianza vizuri tu kwa kuzitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani kabla ya kuitoa na APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
    Kwa upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani. Katika Raundi ya kwanza wakaitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SMG AWAPA ‘TAFU’ LA MAANA YANGA ANGOLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top