• HABARI MPYA

  Sunday, May 15, 2016

  SIMBA YAIKALISHA MTIBWA JAMHURI, AZAM YAICHIMBIA KABURI AFRICAN SPORTS

  Na Saada Mohamed, MOROGORO
  SIMBA SC imeibuka na ushindi wa kwanza baada ya mechi nne za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia kuichapa bao 1-0 Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
  Shujaa wa Simba SC ni kiungo Abdi Hassan Banda aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 70 kwa kichwa akimalizia krosi nzuri ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
  Tangu iifunge 2-0 Coastal Union mjini Tanga, Simba haijashinda mechi nyingine ya Ligi Kuu hadi iliposhinda tena leo.

  Ilifungwa 1-0 na Toto Africans, ikatoa sare ya 0-0 na Azam FC, ikafungwa 1-0 na Mwadui FC zote Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kutoa sare ya 0-0 na Majimaji mjini Songea katikati ya wiki.
  Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 62 baada ya kucheza mechi 29 ikiendelea kukamata nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye pointi 63 na mabingwa Yanga, wenye pointi 72.
  Mchezo mwingine wa ligi hiyo leo, Azam FC imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Mabao ya Azam FC yamefungwa na mshambuliaji Mkenya Allan Wanga dakika ya 10 na beki Erasto Nyoni dakika ya 74, wakati la Sports limefungwa na Omary Ibrahim dakika ya 11.
  Kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Said Mohamed, Shiza Kichuya/Maulid Gole dk72, Dickson Daudi, Shaaban Nditi, Mohamed Ibrahim, Muzamil Yassin, Issa Rashid, Ally Sharrif, Said Bahanuzi/Vincent Barnabas dk55, Hussein Javu/Ally Yussuf dk80 na Andrew Vincent.
  Simba SC; Peter Manyika, Hassan Isihaka, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Mohammed Fakhi, Abdi Banda, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Mussa Hassan Mgosi, Said Ndemla na Peter Mwalyanzi/Said Issa dk84.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAIKALISHA MTIBWA JAMHURI, AZAM YAICHIMBIA KABURI AFRICAN SPORTS Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top