• HABARI MPYA

  Sunday, May 01, 2016

  SIMBA YAIFAGILIA NJIA YA UBINGWA YANGA, YALAZIMISHA SARE 0-0 NA AZAM FC

  Na Saada Mohammed, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imelazimisha sare ya bila kufungana na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Matokeo hayo yatapokewa kwa furaha na mahasimu, Yanga ambao sasa wanaongoza Ligi Kuu kwa wastani wa pointi sita kuelekea mechi nne za mwisho.
  Kwa sare hiyo ya 0-0, Azam FC inafikisha pointi 59, wakati Simba sasa inakuwa na pointi 58, nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 65 baada ya timu zote kucheza mechi 26.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mathew Akrama wa Mwanza, aliyesaidiwa na washika vibendera Abdallah Mrisho wa Pwani na Omar Kambangwa wa Dar es Salaam hakukuwa na mashambulizi ya kusisimua na timu zote zilionekana kucheza kwa tahadari kupita kiasi, hivyo kuufanya mchezo upooze.
  Kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar 'Sure Boy' akipiga mpira kichwa mbele ya kiungo wa Simba, Jonas Mkude leo

  Lakini kipindi cha pili, kilianza kwa mchezo wa kukamiana na kuchezea rafu na undava, jambo ambalo hata hivyo refa Akrama alilidhibiti kwa busara za kuwatuliza wachezaji wa timu zote mbili kwa kuzungumza nao.
  Baada ya hapo, kidogo mchezo wenye hadhi ya timu kubwa katika Ligi Kuu ya nchi, tena zinazowania ubingwa ndiyo ukaanza kuonekana kwa mshambulizi ya pande zote mbili.
  Nahodha wa Azam FC, John Bocco peke yake akakosa mabao mawili ya wazi na kushika kichwa kwa masikitiko, wakati upande wa Simba Hamisi Kiiza na Hajji Ugando walipoteza pia nafasi za wazi.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Emery Nimubona, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid/Brian Majwega dk74, Novart Lufunga, Justise Majabvi, Awadh Juma, Jonas Mkude, Hamisi Kiiza, Danny Lyanga/Hajji Ugando dk54/Mussa Mgosi dk90+2 na Peter Mwalyanzi.
  Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Aggrey Morris, David Mwantika, Jean Mugiraneza/Kipre Balou dk76, Ramadhani Singano ‘Messi’/Mudathir Yahya dk46, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Kipre Tchetche/Ame Ali ‘Zungu’ dk65, John Bocco na Khamis Mcha ‘Vialli’.
  Kikosi cha Azam FC killichoanza dhidi ya Simba SC leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
  Kikosi cha Simba SC killichoanza dhidi ya Azam FC leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAIFAGILIA NJIA YA UBINGWA YANGA, YALAZIMISHA SARE 0-0 NA AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top