• HABARI MPYA

  Thursday, May 19, 2016

  SIMBA SC YAONYESHWA WAKALI WATATU WA KUSAJILI TIMU ITISHE TENA

  Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
  ILI iweze kurejea kwenye ushindani na hatimaye kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara msimu ujao na kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya Afrika mwakani, Simba inatakiwa kusajili wachezaji wazoefu katika nafasi tatu tofauti imeelezwa.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE katika mahojiano maalum, Kocha Mkuu wa zamani wa Yanga na mchambuzi mahiri wa soka, Kennedy Mwaisabula alitaja nafasi ambazo Simba inatakiwa kusajili ni ya kipa ambaye ni mzoefu na atakayekuja kutoa ushindani dhidi ya Vicent Angban kutoka Ivory Coast.
  Mwaisabula alisema kuwa Simba ili iwe imara katika msimu ujao wa ligi inatakiwa kusajili mabeki wa kati wawili wazoefu ambao watasaidia kulinda lango lao lishipate mashambulizi ya mara kwa mara katika mechi mbalimbali watakazocheza.
  Beki wa Simba SC, Novaty Lufunga (kushoto) akijaribu kuzuia shuti la Kahmis Mcha 'Vialli' wa Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu hivi karibuni. Simba imeshauriwa kuwatunza wachezaji wake na kuongeza kadhaa ili wawe na timu tishio msimu ujao 
  Kocha huyo ambaye aliwahi pia kuiongoza Transit Camp iliyoshiriki Ligi Kuu ya Bara alitaja nafasi nyingine ambayo Wekundu wa Msimbazi wanatakiwa kuijaza ni ya safu ya ushambuliaji na hiyo itawafanya kuwa na mfungaji ambaye ataongoza mashambulizi kwa kufunga mabao yatakayoipa ushindi timu hiyo.
  "Kipa wao Mu-Ivory Coast (Angban) anahitaji kupata mpinzani, Manyika (Peter) bado ana utoto mwingi, hata mwaka jana yeye ndiye aliyeimaliza Simba, katika mechi tano kipa hutakiwa kuwa na makosa zaidi ya 16, lakini Manyika kwenye mechi tano anakuwa na makosa mengi mnoooo, wakipata kipa aliyetulia, Simba itasimama," alisema mchambuzi huyo.
  Alisema kuwa kwake haoni kikosi cha Simba kilichoko ni dhaifu, ila klabu hiyo 'ilijiroga' yenyewe pale ilipoomba kusimama mechi zake za ligi na kusisitiza Yanga na Azam FC waliokuwa na mechi za Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho wacheze kwanza 'viporo' vyao.
  "Lile ndiyo lilikuwa kosa la jinai kwa Simba, kusimama kwa siku zaidi ya 14 bila kucheza wakati walikuwa wako kwenye 'form' ndipo walipoharibikiwa, wachezaji wanaoshiriki Ligi ya Tanzania hawajui kujitunza, labda wangewapeleka kambini Afrika Kusini au Lushoto kuwajenga zaidi," Mwaisabula alisema.
  Aliongeza kwamba Simba iliyopo si mbaya na 'majanga' ambayo inayapata ni kwa sababu Yanga imetwaa ubingwa wa ligi na yenyewe bado inapambana kumaliza msimu ikiwa kwenye nafasi ya pili.
  "Kama Yanga ingemaliza kwenye nafasi ya tano, Azam ya pili na ubingwa ungekwenda kwa Mwadui au Ndanda, walakusingekuwa na kelele hizi, hii inatokana na upinzani wa jadi wa klabu hizi kongwe," alisema Mwaisabula.
  Aliwashauri pia viongozi wa Simba kuhakikisha inawabakiza nyota wake walioitumikia msimu huu ili kuiendeleza timu hiyo badala ya kuwaacha na kila mwaka kujenga kikosi kipya.
  "Ameondoka Kessy (Hassan), basi hao wengine wawaangalie vizuri, wakipata na straika mkomavu kama Ngoma (Donald) watakuwa wamejiganga na msimu ujao wapinzani wao watapata tabu," aliongeza.
  Kikosi cha Simba jana asubuhi kilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Polisi uliopo barabara ya Kilwa kwa ajili ya kujiandaa na mechi yake ya kufunga pazia dhidi ya JKT Ruvu itakayofanyika Jumapili jijini Dar es Salaam.
  (Somoe Ng'itu ni mwandishi wa gazeti la Nipashe)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAONYESHWA WAKALI WATATU WA KUSAJILI TIMU ITISHE TENA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top