• HABARI MPYA

  Sunday, May 08, 2016

  SIMBA SC KUIPA YANGA UBINGWA LEO?

  Na Somoe Ng’itu, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwenye viwanja mbalimbali ukiwemo wa Taifa, Dar es Salaam ambako wenyeji Simba SC wataiikaribisha Mwadui FC ya Shinyanga.
  Simba SC inahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili kuendelea kuweka hai matumaini ya ubingwa unaowaniwa pia na Yanga SC, huku Azam FC ikiwa imekwishajifuta kwenye mbio hizo.
  Simba SC ina pointi 58 baada ya kucheza mechi 26 na inaweza kufikisha pointi 70 ikishinda zake zote nne zilizobaki kuanzia wa leo dhidi ya Mwadui FC – maana yake bado ina nafasi ya kuwapiku vinara, Yanga wenye pointi 68 sasa baada ya kucheza mechi 27 katika mbio za taji la Ligi Kuu.
  Simba ikitoa hata sare leo, Yanga wataanza kushangilia ubingwa
  Lakini kama itatoa hata sare leo, mashabiki wa Yanga wataingia mtaani kuanza kushangilia ubingwa - kwani hakutakuwa na timu nyingine yenye uwezo wa kufikisha pointi 68 ilizonazo.
  Mwadui FC yenye pointi 37 za mechi 27, yenyewe haimo kwenye mbio za ubingwa wala hofu ya kushuka, kwani tayari kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amekwishaiweka sehemu salama timu yake.
  Hata hivyo, hiyo haiwazuii kupigania ushindi katika mchezo wa leo kwa ajili ya heshima na pia kumaliza katika nafasi za juu zaidi kwenye msimamo wa Ligi Kuu. 
  Simba SC inaingia kwenye mchezo wa leo ikitoka kucheza mechi tatu mfululizo bila kushinda, baada ya kufungwa na Coastal Union katika Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC) na Toto Africans kabla ya kutoa sare na Azam FC katika Ligi Kuu.
  Kocha Jackson Mayanja anajitahi ushindi katika mchezo wa leo ili kurejesha imani kwa waajiri wake, ambao kwa sasa vichwa vinawauma baada ya kuwa na msimu mwingine mbaya.
  Mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ ana njaa ya mabao akiwa anafukuzana na Amissi Tambwe wa Yanga katika mbio za ufungaji bora wa Ligi Kuu.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo ni kati ya wenyeji Kagera Sugar na Azam FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na Tanzania Prisons dhidi ya Majimaji ya Songea, Uwanja wa Majimaji, Songea, wakati keshokutwa Mbeya City watakuwa wenyeji wa Yanga kwenye Uwanja huo huo wa Sokoine.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUIPA YANGA UBINGWA LEO? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top